1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiTaiwan

Tetemeko la ardhi Taiwan lauwa watu 7 na kujeruhi 800

3 Aprili 2024

Watu wapatao saba wamekufa na wengine zaidi ya 800 wamejeruhiwa baada ya tetemeko kubwa la ardhi kuikumba Taiwan, na kusababisha uharibifu mkubwa wa majengo, miundombinu na barabara, huku juhudi za uokozi zikiendelea.

Majengo yakiwa yamepinda baada ya tetemeko la ardhi kuikumba Taiwan
Majengo yakiwa yamepinda baada ya tetemeko la ardhi kuikumba TaiwanPicha: IMAGO/Newscom/EyePress

Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Taiwan, CWA imesema kuwa tetemeko hilo la ardhi lililotokea mapema Jumatano asubuhi lilikuwa na ukubwa wa 7.4 katika kipimo cha Richter, huku Shirika la Utafiti wa Jiolojia la Marekani, USGS likisema chimbuko la tetemeko hilo ni kilomita 18 kusini mashariki mwa kaunti ya Hualien, katika kina cha kilomita 34.8.

Idara ya Kitaifa ya Zimamoto imeeleza kuwa takribani majengo 26 yameanguka, huku zaidi ya nusu ya idadi hiyo yakiporomoka kwenye kaunti ya mashariki ya Hualien.

Kulingana na idara hiyo, vifo vyote vimetokea katika kaunti hiyo, na kwamba hadi sasa watu 820 wamejeruhiwa. Aidha, ripoti zinaeleza kuwa waokoaji wanatumia ngazi kuwaokoa watu na kuwapeleka maeneo salama.

Maafisa wa uokozi wakiwaokoa watuPicha: AP/picture alliance

Picha na video zilizorushwa kwenye televisheni za Taiwan zimeonyesha maghorofa mengi kwenye kaunti ya Hualien na kwengineko yakiporomoka na kutitia na mengine yakiwa yamepinda, huku ghala katika jiji la Taipei likiwa limebomoka. Meya wa Taipei amesema zaidi ya watu 50 walionusurika walifanikiwa kuokolewa kutoka kwenye vifusi vya jengo hilo.

Mmoja wa wakaazi wa Taipei, Fu Zhong Mei, amezungumza baada ya tetemeko hilo kutokea. ''Nilipodungua kuwa ni tetemeko, haraka nilivaa nguo na viatu, kisha nikamchukua mwanangu tukakimbia na kushuka ngazi. Sijachukua kitu chochote,'' alifafanua Fu.

Tetemeko la ardhi limesikika kote Taiwan

Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Matetemeko cha Taipei, Wu Chien-fu amesema tetemeko hilo limesikika kote Taiwan na kwenye visiwa vya pwani.

Wu amesema umma unapaswa kuzingatia tahadhari na ujumbe unaootolewa na watu wanapaswa kuwa tayari kuondolewa kwenye makaazi yao kutokana na tetemeko la ardhi.

Tetemeko la leo limetokea wakati watu walipokuwa wakielekea makazini na wanafunzi shuleni, hali iliyosababisha tahadhari ya tsunami kutolewa katika pwani za kusini mwa Japan na Ufilipino. Hata hivyo, tahadhari hiyo iliondolewa baadaye. Maafisa wameonya kuhusu uwezekano wa kutokea kwa matetemeko zaidi katika siku zijazo.

Mfanyakazi wa duka akisafisha baada ya tetemeko la ardhi kudondosha vituPicha: AFP

Maafisa wamesema watu 77 bado wamekwama katika njia za chini ya ardhi za Dekalun, huku katika njia za chini ya ardhi ya Chongde kwenye Hifadhi ya Taifa ya Taroko, kundi la watu kadhaa wakiwemo raia wawili wa Ujerumani wamekwama ndani.

Watu zaidi wakwama

Watu wengine 60 wamekwama kwenye njia za chini ya ardhi ya Jinwen, barabara kuu ambayo inaiunganisha miji ya Suao na Hualien.

Wu amewaambia waandishi habari kuwa tetemeko hilo la ardhi ni kubwa kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 25 iliyopita.

Kwa mujibu wa Wu, tetemeko la mwisho lenye ukubwa wa 7.6 katika kipimo cha Richter, lilitokea Septemba 1999, na kuwaua watu wapatao 2,400, hayo yakiwa ni majanga mabaya zaidi ya asili katika historia ya kisiwa hicho.

(AFP, AP, DPA, Reuters)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW