1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiUturuki

Tetemeko la ardhi Uturuki na Syria laangamiza watu 24,000

11 Februari 2023

Wakoaji nchini Uturuki na Syria wameendelea na kazi ya kupekua vifusi kuwatafuta manusura au kuopoa miili ya watu waliopoteza maisha kutokana na tetemeko la ardhi lililoyakumba mataifa hayo mawili siku ya Jumatatu.

Türkei | Erdbeben | Suche nach Verschütteten in Adana
Picha: Teri Schultz/DW

Juhudi hizo zinafanyika wakati idadi ya vifo vilivyosababishwa na janga hilo la asili imepanda na kufikia watu 24,000 huko mamia kwa maelfu wengine wamepoteza maeneo ya kuishi.

Sehemu kubwa ya vifo na athari mbaya kabisa ya tetemeko hilo la ardhi la siku ya Jumatatu imeshuhudiwa kwenye mji wa mashariki mwa Uturuki wa Kahramanmaras.

Mji huo ndiyo ulitikishwa vibaya na zilzala hiyo ya asili iliporomosha majengo, kuharibu miundombinu na kuvuruga kabisa maisha ya watu ambao hadi Jumapili iliyopita walikuwa wakiishi maisha ya kawaida kwenye eneo hilo.

Mji huo unapatikana kwenye mkoa wa pembezoni kabisa mwa Uturuki ambao umekuwa makaazi ya watu waliokimbia machafuko ndani ya Uturuki na nchi jirani ya Syria.

Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuwa karibu watu 870,000 hivi sasa wanahitaji msaada wa haraka wa chakula nchini Uturuki na Syria. Nchini Syria pekee, watu wasiopungua milioni 5.3 huenda wamepoteza maeneo yao ya makaazi.

Watu bado waendelea kupatikana chini ya vifusi wakiwa hai 

Kwenye maeneo ya maafa, miujiza imeendelea kushuhudia hata baada ya saa 100 tangu kutokea kwa tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 7.8 katika kipimo cha Richter.

Picha: BULENT KILIC/AFP

Mwanamke mmoja mjamzito kwa jina la Zahide Kaya amepatikana akiwa hai kutoka kwenye kifusi cha jengo baada ya saa 115 tangu kutokea kwa tetemeko.

Kulingana na shirika la habari la Uturuki, mwanamke huyo ameokolewa kwenye wilaya ya Nurdagi iliyopo katika jimbo la Gaziantep, kusini mashariki mwa Uturuki.

Mtoto wake wa kike mwenye umri wa miaka 6 naye aliokolewa kutoka kwenye vifusi saa moja baadaye. Mama huyo amekutwa na majereha kadhaa mwili na alipelekwa mara moja hospitali.

Hata hivyo hali ya hewa ya baridi kali imesababisha ugumu wa maisha kwa wale walionusurika na hata vikosi vya waokoaji. 

Syria hali bado ni mbaya lakini Uturuki janga hilo lamtikisa rais Erdogan

Wakati hayo yakiripotiwa kwenye eneo la maafa, Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ametoa rai ya kusitishwa mapigano nchini Syria ili kuruhusu msaada kuwafikia manusura wa tetemeko la ardhi.

Picha: DHA/AFP

Watu milioni nne kwenye mkoa unaodhibitiwa na waasi wa kaskazini magharibi mwa Syria wanategemea misaada ya kiutu kuendesha maisha yao lakini hadi sasa hakuna shehena za msaada zilizofika kwa muda wa wiki tatu kutoka maeneo yanayodhibitiwa na serikali mjini Damuscus.

Ni misafara miwili tu iliyobeba msaada ndiyo imelifikia eneo hilo ikitokea Uturuki. Kutokana na wasiwasi huo juu ya hali ya kibadamu nchini Syria, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa  huenda litakutana wiki ijayo kujadili hatua za kuchukua.

Nchini Uturuki mkasa wa tetemeko umesadifu kuwa kaa la moto kwa utawala wa rais Recep Tayyip Erdogan ambaye analaumiwa kila upande kwamba hakufanya vya kutosha kuwasaidia waathirika.

Yeye mwenyewe amelazimika kukiri kwa mara nyingine hapo jana kwamba serikali yake ilishindwa kuwafikia haraka na kuwasaidia waathirika wa tetemeko "kama ambavyo wangetaraji".

Katika wakati kampeni za uchaguzi wa rais zinaendelea inaonesha wapinzani nchini humo wamepata jukwaa la kumsulubu rais Erdogan.