THE HAGUE : Mahkama ya Kimataifa yaamuru kukamatwa kwa kiongozi wa waasi wa LRA wa Uganda na wenzake
14 Oktoba 2005Mahkama ya Kimataifa ya Uhalifu leo hii imevunja lakiri ya hati za kukamatwa kwa wanachama watano wa kundi la waasi la Uganda linaloogopewa la LRA na hiyo kwa mara ya kwanza kabisa kutowa amri ya kulazimisha kufunguliwa kwa mashtaka kisheria na mahkama hiyo ya kudumu duniani ya uhalifu wa vita.
Hati za kukamatwa kwao zimetolewa tarehe nane mwezi wa Julai na kutumwa kwa serikali ya Uganda mjini Kampala lakini zilifanywa siri ili kulinda mashahidi na wahanga.Hati hizo zinamtaja kiongozi wa kundi hilo la LRA Joseph Kony na makamanda wake wanne waandamizi ambao inaaminika wamekimbilia kusini mwa Sudan.
Watuhumiwa hao wanashutumiwa kwa mkondo wa vitendo vya kikatili dhidi ya raia ikiwa ni pamoja na mauaji na kuwateka nyara watoto kwa ajili ya kuwatumia kama watumwa wa ngono na wapagazi.
Vita kati ya waasi hao na serikali ya Uganda vimedumu kwa miaka 19.