1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Theluji yasitisha usafiri Ujerumani

8 Februari 2021

Shughuli za kawaida zimetatizika kaskazini, mashariki na kati mwa Ujerumani kutokana na theluji nzito iliyokwamisha usafiri wakati wiki inaanza.

Winterwetter in Deutschland | ICE im Bahnhof Dortmund
Picha: Ina Fassbender/AFP/Getty Images

Usafiri wa reli na barabara kwenye maeneo mbalimbali ya Ujerumani ulifunikwa kwa theluji. Msimu huu wa baridi, pia umevuruga safari nchini Ubelgiji, Uholanzi na Uingereza, huku theluji zaidi ikitabiriwa katika sehemu nyingi za kaskazini mwa Ulaya.

Polisi katika jimbo North Rhine-Westphalia inasema ilipokea simu 720 za ripoti ya athari za theluji hiyo katika kipindi cha saa 24 siku ya Jumapili.

Kulingana na kituo cha taifa cha udhibiti wa majanga maafisa waliitwa kwa kesi 507 za ajali zinazohusiana na hali ya hewa kuanzia saa 12 asubuhi siku ya Jumatatu.

Picha: Reuters/M. Dalder

Ajali barabarani

Miongoni mwa ajali zilizotokea kumeripotiwa kifo cha mtu mmoja na watu wengine 37 waliopata majeraha kidogo. Hii ni baada ya gari lililokuwa likiendeshwa kwa kasi kupoteza mwelekeo na kudumbukia kwenye mto mdogo, dereva wa gari hilo alipoteza maisha huko Duisburg.

Mjini Dortmund Polisi imesema wamepokea simu kupita kiasi na wamewaomba watu kusalia nyumbani mpaka hali ya hewa itakapo kuwa shwari.

"Tumieni fursa ya kufanyia kazi nyumbani na uwezekano mwingine ili msiongeze msongamano barabarani," imesema taarifa ya polisi.

Huduma za usafiri kwa njia ya reli Ujerumani katika maeneo ya Berlin na Hamburg ziliathirika zaidi.

Usafiri umehairishwa

Shirika la Reli la Ujerumani la Deutsche Bahn limeahirisha safari za kuelekea katika miji ya Hanover, Cologne, Frankfurt na Munich.

Mwandishi wa DW Jared Reed amesema licha ya kuhairishwa kwa safari nyingi hakukuwa na watu wengi ambao walikwama Hanover eneo kubwa linalounganisha treni za masafa marefu za Ujerumani.

Nchini Uholanzi, mamlaka iliamua kutangaza hali ya hatari wakati taifa hilo likikabiliana na theluji kali zaidi katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja.

Picha: Getty Images/P. Guelland

Safari nyingi za ndege zilichelewa na nyengine zilihairishwa katika uwanja wa ndege wa Schiphol, huku shughuli za uwanja wa ndege uliopo kusini mwa Uholanzi Eindhoven ukifuta kabisa huduma zake.

Uingereza pia ilitarajia theluji kubwa kutoka kwa mfumo wa hali hewa ambao wataalamu wa hali ya hewa wanauita "Storm Darcy".

 

https://p.dw.com/p/3p2lN