1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Theresa May aitisha uchaguzi wa mapema

Sekione Kitojo
18 Aprili 2017

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May ametangaza kuitisha uchaguzi wa mapema ifikapo Juni 8, akisema anahitaji kuimarisha uungwaji mkono katika mazungumzo ya Uingereza kujitoa Umoja wa Ulaya.

Theresa May
Picha: Getty Images/D.Kitwood

Akisimama  nje  ya  ofisi  yake  katika  mtaa wa  Downing, May alisema  alisita  juu  ya  kuliomba  bunge  kuunga  mkono  hatua yake  hiyo  kuitisha  uchaguzi  na  mapema, kutoka  mipango  ya awali  ya  kuitisha  uchaguzi  huo  mwaka  2020, lakini  aliamua  ni muhimu  kupata  uungwaji  mkono  kwa  juhudi  za  chama  chake tawala  cha  Conservative  kuendelea  na  hatua  za  Uingereza kujitoa  kutoka  Umoja  wa  Ulaya. Baadhi  wameshangazwa  na hatua  yake, amekuwa  akisema  mara  kwa  mara  hataki kuvurugwa  na  kampeni itakayopoteza  muda, lakini  uchunguzi  wa maoni  ya  wapiga  kura  unamuonesha  akiwa  anaongoza, uchumi unakwenda  vizuri  licha  ya   kura  ya  Brexit na  amekabiliana  na upinzani  kutoka  katika  chama  chake  binafsi  kutokana  na mageuzi  ya  ndani.

Sarafu  ya  pauni  imepanda  kwa  kiwango  cha  juu  cha  miezi miwili  na  nusu  dhidi  ya  dola  ya  Marekani  baada  ya  kutangaza uchaguzi, lakini  faharasa  kuu  ya  soko  la  hisa  nchini  Uingereza iliporomoka  katika  kiwango  chake  cha  chini  kabisa  katika  muda wa  zaidi ya  wiki  saba. Uingereza  inajiunga  na  orodha  ya  nchi kadhaa  za  Ulaya  zinazopanga  kufanya  uchaguzi mwaka  huu. Uchaguzi  nchini  Ufaransa  mwezi  Aprili  na  Mei  na  Ujerumani mwezi  Septemba  una uwezekano  wa  kuelekeza  taswira  ya kisiasa  katika  miaka  miwili  ijayo  ya  majadiliano  ya  Uingereza kujitoa  kutoka  Umoja  wa  Ulaya wakati  mazungumzo  yanatarajiwa kuanza  rasmi  katika  mwezi  wa  Juni.

Wapinzani wa Labour mashakani

Wajumbe  wa  majadiliano  wa  Umoja  wa  Ulaya  wanamatumaini kwa  hatua  hiyo  ya  waziri  mkuu  wa  Uingereza  itampa  nguvu zinazostahili  akiwa  na  mamlaka  ya  wazi  kuweza  kutoa  masharti ya uingereza  kujitoa  kutoka  Umoja  huo.

Waziri  wa  mambo  ya  kigeni  wa  Ujerumani  Sigmar Gabriel amesema  ana  matumaini  uchaguzi  wa  mapema  utaelekeza katika  uwazi  na  uwajibikaji  katika  majadiliano  ya  Uingereza pamoja  na  umoja  wa  Ulaya  kuhusiana  na  Brexit.

Jeremy Corbyn, mwenyekiti wa chama cha Labour Picha: picture-alliance/PA Wire/empics

Kiongozi  wa  chama  kikuu  cha  upinzani  nchini  Uingereza  cha Labour, Jeremy Corbyn  amesema  anaupokea uamuzi  wa  waziri mkuu  May. "Naikaribisha  fursa  hii, kwetu  sisi  kuweza  kuwaeleza Waingereza  kusimama  dhidi  ya  serikali  hii  na  ajenda  yake iliyoshindwa   ya  kiuchumi, ambayo  imesababisha  matatizo  katika huduma za  afya, mashule  kupata  fedha  chache, pamoja  na kuwaacha  watu  wengi hawana  hakika. Tunataka kuwaelezea wananchi  wa  Uingereza, kuhusu jamii inayomjali  kila  mtu, uchumi unaofanyakazi  kwa  kila  mtu, na  Brexit inayofanyakazi  kwa  kila mtu."

Nae waziri kiongozi  wa  Scotland Nicola Sturgeon  amesema  hatua ya  waziri  mkuu  May  inaakisi  dhamira  yake  kuipeleka  Uingereza katika mrengo  wa  kulia  wa  kisiasa  wakati  nchi  hiyo  ikijadili kuhusu  Brexit  kutoka  Umoja  wa  Ulaya. Sturgeon  amesema  May anachukua  fursa  ya  mtafaruku  mkubwa  katika  chama  cha Labour  ili  kuzima  upinzani na  kuwatenga  watu  ambao wanampinga. "Hatua  hii itakuwa  na  maana  sio tu  uwezekano mgumu  wa  Brexit, lakini  kubana  zaidi  matumizi na upunguzaji mkubwa wa bajeti. Kwa  hiyo katika  Scotland ni  muda  sasa  wa kuhakikisha  kwamba  tunasimama kwa  ajili  ya  maslahi  ya Scotland, kuifanya  sauti  ya  Scotland  kusikka na  kuhakikisha wabunge  wanapigania  maslahi  ya  Scotland."

Utaratibu  wa  serikali  nchini  Uingereza  kuitisha  uchaguzi mpya una utata  mkubwa  kuliko  ilivyozoeleka  hapo  kabla. Serikali zilikuwa  na  uwezo  wa  kuitisha  uchaguzi kama  zitakavyo, lakini sheria ya  bunge  ya  muda  maalum, iliyopitishwa  mwaka  2021 , imeweka  vipindi  maalum kufanyika  uchaguzi  kila  baada  ya  miaka mitano. Chini  ya  sheria  hiyo, hoja  ya uchaguzi  mpya  kabla  ya wakati  inapaswa  kupelekwa  bungeni  na  kukubaliwa  na  theluthi mbili  ya  wabunge  650  katika  baraza  la  wawakilishi, ikiwa  ni pamoja  na  viti ambavyo  havina  wabunge. May  amesema atawasilisha  hoja  hiyo bungeni  kesho Jumatano. Iwapo  itapita, bunge  litasitisha  shughuli  zake  siku 25 kabla  ya  siku  ya Uchaguzi.

Mwandishi: Sekione  Kitojo/rtre

Mhariri: Grace Kabogo

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi

Gundua zaidi

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW