1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Theresa May atoa wito kwa wapinzani kuhusu mpango wa Brexit

John Juma AFPE, APE, RTRE
17 Januari 2019

Baada ya mpango wake wa Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya kukataliwa bungeni na yeye pia kuponea kura ya kutokuwa na imani naye, Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May sasa anajaribu kuwashirikisha wapinzani.

Großbritannien Ansprache Theresa May nach Misstrauensvotum
Picha: Reuters/C. Kilcoyne

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May leo anakabiliwa na mkwamo mwingine kuhusu mpango mpya wa mchakato wa Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya - Brexit. Hii ni baada ya May kupata ushindi mdogo kwenye kura ya kutokuwa na imani naye, kufuatia kushindwa kwa mpango wa awali wa Brexit.

Bibi May anayekabiliwa na shinikizo kubwa, alikubali kuwa makubaliano aliyoyafikia na Umoja wa Ulaya, yamekataliwa, baada ya serikali yake kupata pigo kubwa la kihistoria katika taifa hilo. May na waliounga mkono mpango wake, walipata kura 202 pekee huku walioupinga wakipata kura 432 bungeni.

Huku muda ukizidi kwenda mbio, bibi May amewatolea wito viongozi wa upinzani kukutana naye kwa mazungumzo ya pamoja ya vyama vyote vya kisiasa, kabla ya kuwasilisha pendekezo mbadala kwa bunge la nchi hiyo siku ya Jumatatu wiki ijayo. May amesema

"Makubaliano niliyoafikiana na Umoja wa Ulaya yamekataliwa na wabunge , tena kwa kiasi kikubwa. Ninaamini ni wajibu wangu kutimiza takwa la Waingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya na ninanuia kufanya hilo. Kwa vile wabunge wameweka wazi kile wasichokitaka, ni lazima tushirikiane pamoja kupata kile bunge linachotaka."

Upinzani waweka masharti

Kiongozi wa chama cha Labour Jeremy Corbyn amesema atashauriana tu na Theresa May kuhusu mpango mbadala kwa masharti.

Lakini wapinzani wake wamewasilisha orodha ya matakwa yao ili kuwezesha ushirikiano na May, ikiwemo kufuta uwezekano kwamba Uingereza itaweza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya mwezi Machi bila ya makubaliano kabisa.

Theresa May amesema amesikitishwa na uamuzi wa kiongozi wa chama cha Labour Jeremy Corbyn kukataa kushiriki katika mashauriano naye. Hata hivyo bibi May amesema milango bado iko wazi kwa yeyote kushiriki.

Mwenyekiti wa chama cha kihafidhina cha Theresa May, Brandon Lewis amesema kufuatia hali ya sasa ya Uingereza, kuwa nchi hiyo haiwezi kuwa katika umoja wa forodha na Jumuiya ya Ulaya kwa sababu kusaini mikataba ya biashara baada ya Brexit ni suala linalopewa kipaumbele.

Wanachama wa Umoja wa Ulaya wajadiliana kuhusu hatua za kuchukua

Hayo yakijiri nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya pia zinajadiliana kuhusu namna ya kusonga mbele baada ya bunge la Uingereza kuyakataa makubaliano ya May kuhusu Brexit.

Uingereza inatarajiwa kujiondoa katika Umoja wa Ulaya ifikapo Machi 29.

Mwandishi: John Juma

Mhariri: Iddi Ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW