1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Theresa May aunda baraza lake la mawaziri

Admin.WagnerD14 Julai 2016

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May ameendelea kuliunda baraza lake la mawaziri leo, akiweka pamoja serikali yake ambayo imewaweka kando wengi ya waliokuwa wakimuunga mkono mtangulizi wake David Cameron.

Kombi-Bild Theresa May Boris Johnson
Theresa May (kushoto)na Boris Johnson waziri wa mambo ya kigeni wa uingereza(kulia)

katika uteuzi wake amewaweka watu ambao wanapinga kwa nguvu zote Umoja wa Ulaya katika majukumu mazito ya kimataifa.

Baada ya kupanga kiasi ya nusu darzeni ya nyadhifa za juu jana , ikiwa ni pamoja na uteuzi wa kushangaza wa Boris Johnson kuwa waziri wa mambo ya kigeni, waziri mkuu Theresa May alifanya uteuzi mpya leo, ikiwa ni pamoja na waziri wa sheria Liz Truss na waziri wa elimu Justine Greening.

Michael Gove waziri wa zamani wa sheria katika serikali ya David CameronPicha: Getty Images/C. Furlong

Pia amewaondoa mahasimu, akiwafuta kazi washirika wa serikali ya waziri mkuu mstaafu David Cameron ikiwa ni pamoja na waziri wa utamaduni John Whittingdale, waziri wa elimu Nicky Morgan na hususan, waziri wa sheria wa zamani Michael Gove, mmoja kati ya mahasimu wake katika kinyang'anyiro cha kuwania kuwa kiongozi wa chama cha Conservative na hatimaye kuingia jengo namba 10 mtaa wa Downing.

Wasaliti

Gove aliongoza kampeni ya "kujitoa" katika kura ya maoni kuhusu Umoja wa Ulaya, pamoja na meya wa zamani wa London Boris Johnson , na kisha akamgeuka kwa kuwania uongozi wa chama cha Conservative, wadhifa ambao Johnson aliuwania kwa muda mrefu.

Boris Johnson na Theresa May(kulia)Picha: Getty Images/A. Matthews

May alishinda vita vya kuwania kuchukua madaraka na kisha haraka akamtupa kando Gove, ambae hivi sasa anaonekana kuwa msaliti na wengi wa wanachama wa chama cha Conservative. Amemzawadia Johnson kwa kumpa kazi hiyo yenye umaarufu ya waziri wa mambo ya kigeni.

Kejeli na muongo

Akionekana kuwa muongo na waziri mwenzake wa Ufaransa na kukejeliwa kwamba ni kichekesho cha kisiasa , na magazeti barani Ulaya , kiongozi huyo wa kampeni ya Brexit Boris Johnson anakabiliwa na wimbi la ukosoaji na kejeli baada ya kuteuliwa kuwa waziri wa mambo ya kigeni.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa Jean-Marc AyraultPicha: picture-alliance/dpa/D. Van Tine

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa Jean-Marc Ayrault amedai kwamba hana wasi wasi juu ya kufanyakazi pamoja na Johnson lakini amesisitiza haja ya kuwa na mshirika , wa uhakika,mwenye kuaminika na wakutegemewa.

"Sina wasi wasi kuhusu Boris Johnson,nafahamu kuhusu utaratibu wake ulivyo na mbinu zake.Wakati wa kampeni aliwadanganya mno Waingereza na sasa ni yeye ambae mgongo wake uko ukutani. Anatakiwa kuitetea nchi yake, wakati yuko ukutani. Kwa hiyo uhusiano huu na Ulaya unapaswa kuwa wa wazi."

Uhasama ni mkubwa katika mataifa ya Ulaya kuhusiana na Johnson , ambae hivi karibuni alifananisha malengo ya Umoja wa Ulaya na yale ya Adolf Hittler.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry (kushoto) na Federica Mogherini wa Umoja wa UlayaPicha: picture-alliance/AA/D. Aydemir

Serikali nyingi , zikifuata itifaki , zimempongeza waziri mwenzao huyo mpya , ambaye ataanza rasmi kazi yake ya kidiplomasia mjini Brussels wiki ijayo.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry alimpigia simu mwenzake huyo wa Uingereza leo na mawaziri hao wawili wameakubaliana kwamba uhusiano maalum kati ya Marekani na Uingereza ni muhimu kuliko wakati mwingine wowote.

Mwandishi Sekione Kitojo / afpe /rtre / ape

Mhariri: Mohammed Khelef