Theresa May azidi kuzongwa kuhusu Brexit
16 Novemba 2018Baada ya siku ya jana iliyokuwa na vurumai ambapo mawaziri walijiuzulu na wanachama wa chama chake kupanga njama za kumuondoa madarakani, May alikabiliana na umma kutetea msimamo wake , katika kipindi cha redio ambamo watu walipiga simu kumuuliza maswali.
Kiongozi huyo wa chama cha Conservative alisema kuwa anaamini kila sehemu ya mwili wake kuhusu mwelekeo wa Brexit ambao ameupanga, baada ya kukabiliana na bunge hasimu na kushuhudia mawaziri wanne , ikiwa ni pamoja na waziri anayehusika na Brexit Dominic Raab, wakijitoa kutoka katika serikali yake. Wabunge kutoka pande zote walimuonya kwamba hakuna uwezekano wowote ambapo mpango wake unaweza kupata uungwaji wao mkono, lakini alipuuzia miito ya kutaka ajiuzulu, akisema, "nitahakikisha hili linafika mwisho".
Waziri mkuu amekiri kuwapo na "wasiwasi kuhusu suluhisho la muda mfupi " kuhusiana na suala la mpaka na Ireland katika makubaliano hayo, ambapo wanaounga mkono Brexit wanahofu litaifunga Uingereza bila ukomo katika umoja wa forodha.
Kura ya pili ya maoni
Wakosoaji wanaamini May amekubaliana katika mambo mengi na Umoja wa Ulaya katika maeneo muhimu, wakati waounga mkono kubakia katika Umoja wa Ulaya wanatoa wito wa kufanyika kura ya pili ya maoni kuhusu makubaliano ya mwisho.
"Nimechukua mtazamo wa wazi juu ya suala la kura ya maoni ya pili, nimeweka wazi kwa wabunge. Na nafikiri wengi wa wabunge wanatambua wamewapa fursa wananchi wa Uingereza kupiga kura na wananchi wameamua, ni juu yetu kutimiza kuhusu kura hiyo na sio kura ya pili ya maoni. Kwa kadiri ninavyoamini, hakutakuwa na kura ya pili ya maoni."
Waziri wa mazingira Michael Gove, mmoja kati ya watu muhimu katika kampeni ya kuunga mkono Brexit katika kura ya maoni ya mwaka 2016 kuhusiana na uanachama wa Uingereza katika Umoja wa Ulaya , alikataa ombi la kuchukua nafasi ya Dominic Raab na anatafakari kuhusu msimamo wake, kwa mujibu wa ripoti za vyombo kadhaa vya habari.
Mamia kadhaa ya watu waliandamana nje ya bunge mjini London jana wakidai kufanyika kura ya pili ya maoni kuhusu Brexit .
Waandamanaji , wengi wao kutoka chama cha siasa za wastani kinachopendelea kubakia katika Umoja wa Ulaya cha Liberal Democrats kimeeleza kutoridhishwa na mswada wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya waziri mkuu May na Umoja wa Ulaya katika masharti ya Uingereza kujitoa kutoka Umoja huo. Nacho chama cha Ireland ya kaskazini cha Democratic Unionist , ambacho wabunge wake 10 wamemsaidia May kuwa na wingi mdogo bungeni , kinasema kitapiga kura dhidi ya makubaliano hayo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman