1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Thunberg, miongoni mwa washindi wa 'Tuzo Mbadala ya Nobel'

Daniel Gakuba
5 Desemba 2019

Mwanaharakati chipukizi wa kutetea mazingira, Greta Thunberg ni miongoni mwa watu wanne waliotunukiwa Tuzo Mbadala ya Nobel ya haki za Binadamu. Wengine ni wanaharakati kutoka Sahara Magharibi, Brazil na China.

Stockholm Alternativer Nobelpreis
Davi Kopenawa (kulia) kutoka Brazil akipokea Tuzo Mbadala ya NobelPicha: picture-alliance/TT/E. Simander

Jopo linalochagua washindi wa tuzo hiyo wamemsifu Thunberg kama mtu aliyehamasisha na kukuza shinikizo dhidi ya wanasiasa ili wachukue hatua za dharura zinazoendana na ukweli unaoelezwa na wanasayansi kuhusu kitisho cha mabadiliko ya tabianchi.

Pamoja na Greta Thunberg, washindi wengine wa tuzo hiyo mbadala ya Nobel ya haki za binadamu mwaka huu wa 2019 ni  Guo Jianmei, mtetezi wa haki za wanawake nchini China, Aminatou Haidar, shujaa wa kutetea uhuru wa Sahara Magharibi kwa njia ya amani na Dave Kopenawa, mwanaharakati wa haki za Wabrazil asilia. Kila mmoja wao alipokea tuzo ya Kronor za Sweden milioni moja, sawa na takriban dola  laki moja za Kimarekani, pamoja na sanamu ya chuma kutoka mpango wa kuharibu bunduki katika ukanda wa Amerika ya Kati.

Greta Thunberg, mwanaharakati wa kutetea mazingiraPicha: epd/P. Piel

Greta Thunberg avuka Atlantiki kwa boti

Greta Thunberg ambaye ni binti wa miaka 16 hakuwepo mjini Stockholm mahali tuzo hiyo ilipotangazwa jana jioni, alikuwa nchini Ureno alikowasili baada ya safari ya wiki tatu ya kuvuka bahari ya Atlantiki kwa boti, akielekea katika mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, unaofanyika mjini Madrid Uhispania. Lakini alituma ujumbe wa shukrani kwa njia ya video, akiahidi kuendeleza juhudi alizozianzisha.

Soma zaidi: Mkulima wa Burkina Faso ashinda Tuzo mbadala ya Nobel

''Nasikitika kwamba sikuweza kuwa nanyi usiku huu, natmani ningekuwepo. Hivi sasa niko mjini Lisbon, na nashukuru sana kwa heshima niliyopewa ya kutuzwa Tuzo ya ''Haki ya Maisha Bora''. Ina umuhimu mkubwa sana kwangu. Nawatakia jioni njema, na naam, mapambano hayatosimama.'' Alisema binti huyo mwanaharakati.

Aminatou Haidar, mwanaharakati wa kutetea uhuru wa Sahara Magharibi kwa njia ya amaniPicha: picture-alliance/TT/E. Simander

Vuguvugu lililoenea kote duniani

Greta Thunberg alianzisha mgomo wa kwenda shule na kuketi mbele ya bunge la Sweden Agosti mwaka 2018, hatua iliyoanzisha vuguvugu la vijana duniani kote lililopachikwa jina la Ijumaa kwa Mustakabali wa dunia.

Soma zaidi: Kilio cha vijana wa dunia dhidi ya mabadiliko ya tabianchi 

Alipokuwa akitangaza jina la Greta Thunberg kama mshindi wa tuzo hiyo mwaka huu, Johan Rockstrom kutoka Taasisi ya Mabadiliko ya Tabianchi ya mjini Potsdam nchini Ujerumani, alisema vijana ni kama nuru katika shimo lenye giza.

Guo Jianmei, mtetezi wa haki za wanawake nchini ChinaPicha: Imago Images/UPI

Washindi waliohudhuria hafla ya kutoa tuzo hiyo mjini Stockholm Aminatou Haidar na Davi Kopenawa, walitumia hotuba zao za kuikubali tuzo, kuhimiza uungwaji mkono wa kimataifa kwa harakati zao.

Kwa muda wa miaka 30 Bi Haidar amekuwa akiendesha mapambano ya amani ya kudai uhuru wa Sahara Magharibi ambayo inakaliwa na Morocco tangu kuondoka kwa wakoloni wa Uhispania mwaka 1975. Kopenawa kutoka jamii asilia ya Yonamami nchini Brazil, ameunda shirika la kulinda msitu wa Amazon nchini mwake.

Gao Jianmei, mwanasheria kutoka China ambaye analo shirika linalotoa ushauri wa kisheria kwa wanawake bila malipo, yeye pia hakuwepo mjini Stockholm.

dpae, ape

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW