1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tikhanovskaya: Lukashenko sio rais halali wa Belarus

9 Septemba 2020

Kiongozi Mkuu wa upinzani wa Belarus Svetlana Tikhanovskaya amesema Rasi Alexander Lukashenko sio tena rais halali wa taifa hilo machoni mwa raia wake, akisisitiza uchaguzi mpya ndio njia pekee ya kuliokoa taifa hilo

Lithauen Vilnius | Sviatlana Tsikhanouskaya
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Kulbis

Akizungumza mjini Warsaw, Poland, kiongozi huyo aliye uhamishoni nchini Lithuania amesema watu wa Belarus hawatosahau wala kusamehe matukio yalitokea kati ya tarehe 9 10 na 11 wakati walipomiminika barabarani kutaka haki yao.

Amezungumza akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa Poland Mateusz Morawiecki, ambaye katika mkutano huo alimkabidhi Tikhanovskaya ufunguo wa jengo moja mjini humo ambalo ndilo litakalokuwa makao mapya ya Belarus iliyopewa jina la "nyumba ya Belarus"

Svetlana Tikhanovskaya pia ameitolea mwito Urusi  kuwacha kampeni yake ya propaganda na kuunga mkono vuguvugu la kudai demkokrasia nchini Belarus. Amesema uwongo unaosemwa na vyombo vya habari vya Urusi unahatarisha uhusiano mzuri uliopo kati ya watu wa mataifa hayo mawili.

Soma pia: Belarus: Lukashenko asema haondoki ng'o madarakani

"Tusikubali propaganda ziharibu mahusiano kati ya mataifa haya rafiki, na tusikubali pia viongozi wa kisiasa wasiosema ukweli kuharibu maslahi ya watu wa Belarus na Urusi. Waunge mkono watu wa Belarus," alisema Tikhanovskaya.

Viongozi wakuu wa upinzani Maria Kolesnikova na Maxim ZnakPicha: picture-alliance/dpa/Tass/S. Bobylev

Viongozi zaidi wa upinzani wakamatwa na wengine kulazimishwa kuihama nchi

Huku hayo yakiarifiwa, serikali ya Belarus hii leo imemkamata mjumbe wa mwisho wa ngazi za juu wa  mwisho wa Baraza la Upinzani aliyekuwa bado yuko huru, ikinuia kumaliza maandamano ya mwezi mmoja sasa, dhidi ya Rais Alexander Lukashenko.

Mmoja ya wanachama wa upinzani Gleb German, amesema wakili Maxim Znak, mjumbe wa Baraza la Uratibu lililoundwa na upinzani kusimamia mazungumzo kati yao na Rais Lukashenko juu ya hatua za kukabidhi madaraka, alichukuliwa kutoka katika ofisi za baraza hilo na watu wasiojulikana na waliokuwa wamefunika nyuso zao. Gleb amesema Znak alikuwa na muda wa kuandika neno "barakowa", akimaanisha watu waliomchukua walikuwa wamefunika nyuso zao kabla ya kuchukua simu yake. 

Soma pia: Belarus:Kiongozi wa upinzani akamatwa katika mpaka na Ukraine

Wakati hyo yakiendelea, waendesha mashtaka wa serikali wameanzisha uchunguzi wa jinai dhidi ya wajumbe wa baraza hilo wakiwashutumu kwa kuyumbisha usalama wa taifa kutokana na hatua yao hiyo ya kutaka makabidhiano ya madaraka. Wajumbe kadhaa wa baraza hilo walikamatwa na wengine kufukuzwa kwa lazima nchini humo.

Marekani inafikiria kuiwekea vikwazo zaidi Belarus

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Mike PompeoPicha: Getty Images/M. Ngan

Maria Kolesnikova, mmoja wa viongozi wakuu wa upinzani nchini humo, alikamatwa siku ya Jumatatu katika mji mkuu Minsk pamoja na wenzake wawili na kusafirishwa Jumanne asubuhi katika mpaka wa nchi hiyo na Ukraine na kulazimishwa kuingia huko. Kolesnikova anasemekana kuichana hati yake ya kusafiria alipofika eneo la mpakani ili kupinga hatua hiyo na kwa sasa anashikiliwa na serikali ya Belarus lakini hajulikani hasa aliko kiongozi huyo wa upinzani.

Lukashenko amewaita wafuasi wa upinzani kama vibaraka wa mataifa ya Magharibi na kupinga matakwa ya Marekani na Umoja wa Ulaya kushiriki mazungumzo na waandamanaji, wasioutambua ushindi wake katika uchaguzi wa Agosti 9 na kusema ulikumbwa na udanganyifu na haukuwa wa huru na haki huku wakimtaka ajiuzulu.

Soma pia: Maelfu waandamana tena huko Belarus dhidi ya Lukashenko

Kwa upande wake waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Mike Pompeo amelezea wasiwasi wake juu ya jaribio la kumfukuza Kolesnikova nchini Belarus na kuonya kuwa Marekani na washirika wake wanafikiria kuiwekea vikwazo zaidi taifa hilo lililowahi kuwa sehemu ya Muungano wa Kisovieti.

Chanzo: ap/afp/dpa

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW