1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Werner kujiunga na Chelsea

Deo Kaji Makomba
5 Juni 2020

Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ujerumani Timo Werner yuko mbioni kujiunga na Chelsea na sio Liverpool katika ligi kuu ya Premier nchini England.

Fußball Bundesliga |  Schalke 04 v RB Leipzig | Timo Werner
Picha: Getty Images/Bongarts/A. Grimm

Kwa hivi sasa Werner yuko katika maandalizi ya kuondoka katika klabu yake ya RB Leipzig kuelekea England katika kipindi cha majira ya joto lakini kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya Uingereza na Ujerumani zilizochapishwa Ijumaa tarehe 05.06.2020, mshambuliaji huyo ataingia kandarasi ya kuichezea klabu ya Chelsea na sio Liverpool ambako inaonekana kuwa mwisho wa safari yake.

Gazeti la The Bild la Ujerumani, jarida la Kickers sports na magazeti ya Uingereza ikiwemo The Guardian yameripoti kuwa, klabu ya Chelsea walikuwa tayari kulipa kitita cha euro milioni 60 sawa na dola za Kimarekani milioni 68 kama ilivyoanishwa kwenye kifungu cha mkataba wake wa sasa kilichoweka kwa ajili ya kumruhusu mshambuliaji huyo kuondoka ambacho kinatakiwa kutumika kabla ya Juni 15.

Werner mwenye umri wa miaka 24, ana mkataba hadi mwaka 2023 katika klabu ya RB Leipzig ambapo amekwishaifungia klabu hiyo mabao 25 katika ligi kuu ya kandanda ya Ujerumani Bundesliga msimu huu unaoelekea ukingoni na jumla ya mabao 31 katika mashindano yote kwa timu hiyo iliyofuzu kucheza robo fainali ya mashindano yote ya ligi ya mabingwa wa soka barani Ulaya.

Mshambuliaji huyo alihusishwa kwa muda mrefu na hoja ya kuelekea kwa vinara wa ligi kuu ya soka ya England klabu ya Liverpool na meneja wake wa Ujerumani Juergen Klopp, lakini iliripotiwa kuwa Liverpool haikuwa tayari kulipa kiasi hicho kikubwa cha pesa huku kukiwa na sekeseke la mripuko wa virusi vya Corona.

kulingana na ripoti za vyombo vya habari, Werner yuko mbioni kusaini mkataba wa miaka mitano katika klabu ya Chelsea inayoongozwa na kocha Frank Lampard ambaye tayari ana mchezaji wa timu ya taifa ya Ujerumani, beki Antonio Ruediger.

Gazeti la The Guardian limeripoti kuwa klabu ya Chelsea imekuwa na mazungumzo yenye tija na Werner na jarida la Kicker limeripoti kuwa uhamisho wa mchezaji huyo utakamilika wiki ijayo.

Lampard ana mipango wa kuisuka safu ya ushambuliaji ya Chelsea na tayari wamekwishanyakua saini ya Hakim Ziyech kutoka klabu ya Ajax Amsterdam kwa kitita cha euro milioni 40.

Klabu ya Chelsea yenye masikani yake Stamford Bridge inalenga kutumia kiwango kikubwa cha pesa baada ya kutokuruhusiwa kufanya uhamisho katika kipindi kilichopita cha majira ya joto kwa sababu ya marufuku iliyowekwa na bodi ya utawala ya shirikisho la soka barani Ulaya, UEFA, na pia hawakuweza kusajili mchezaji yeyote mnamo mwezi Januari.

Awali Werner alihusishwa katika tetesi za kujiunga vinara na mabingwa wa ligi kuu ya kandanda ya Ujerumani Bundesliga, Bayern Munich, lakini aliwapuuza, na kuliambia gazeti la Bild kwamba "kuchukua maamuzi ya kwenda nje ya nchi itakuwa ni tija zaidi kwangu kuliko kuhamia Bayern."

Na Deo Kaji Makomba/dpa

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW