Timu 9 mbioni kuwania ubingwa Bundesliga
21 Oktoba 2019Mchezo wa nane wa Bundesliga umetoa matokeo yasiyoonesha mwelekeo halisi wa ligi hiyo baada ya vigogo wa ligi kupokea vipigo na kushikwa shati , hali inayoelezea ugumu wa ligi msimu huu. Baada ya kutoka sare mara tatu mfululizo makamu bingwa Borussia Dortmund ilijikakamua na kupata ushindi wa kibarua wa bao 1-0 dhidi ya Borussia Moenchengladbach siku ya Jumamosi na kumpa kocha wa Dortmund pamoja na wachezaji nafasi ya kupumua baada ya ukosoaji mkubwa dhidi ya kikosi hicho jinsi kinavyocheza. Dortmund ilitangaza mwanzoni mwa msimu kuwa mara hii ina nia ya kulinyakua taji la ubingwa wa Bundesliga. Lakini hali yake ya kusuasua imeweka kiwingu katika dhamira hiyo.
Nahodha wa Borussia Dortmund Marco Reus anakiri kuwa ushindi huo umeleta ahueni katika kikosi.
"Baada ya wiki tatu, nne ambamo tulipata matokeo ya sare, shinikizo bila shaka lilikuwapo, katika mchezo wetu huu. Tumeshuhudia pia, kwamba si kwa bahati kuwapo katika nafasi za juu. Naamini kwamba mchezo huu ulikuwa na tofauti ndogo sana kwa kila upande na ungeweza pia kwenda upande mwingine. Lakini mara hii bahati kidogo ilikuwa upande wetu na leo tumefaidika kutoka na jinsi tulivyoweka bidii, na kwamba hatukukata tamaa, tuliendelea kujiamini na mwishowe tumeshinda."
Mchezaji wa kati wa Borussia Moenchengladbach Christoph Krammer, lakini anasikitika kwa timu yake kukosa ushindi licha ya juhudi kubwa , na pia akilamikia maamuzi kwamba wakati mwingine yalikuwa yakienda dhidi yao.
"Tulipata nafasi nyingi sana, lakini kila mara kulikuwa na mguu wa mchezaji wa Dortmund katika sekunde ya mwisho. Si makosa ya kutoweka mbinyo zaidi ama kupoteza umakini, hilo ni suala mara nyingine la bahati tu ama mkosi. Na katika sehemu nyingine, ilikuwa ni kutokana na uamuzi unaoweza kwenda huku ama kule, ama pengine penalti ama sio. Pambano la Hummels dhidi ya Hermann, nafikiri, inawezekana bila shaka ikawa penalti. Lakini hatuwezi kutoa lawama nyingi. Tulipata nafasi saba, ama nane nzuri sana dhidi ya Dortmund, ambazo tungeweza kirahisi kuuweka mpira wavuni, kwa kuwa nafasi zilikuwa nyingi za kuweza kushinda mchezo huo."
Mbali ya vuta nikuvute hiyo kati ya Borussia Moenchengladbach ambayo inashilikilia bado nafasi ya uongozi wa ligi kwa kuwa na pointi 16, dhidi ya Borussia Dortmund yenye pointi 15 , lakini pambano lililokuwa gumzo ni kati ya mabingwa watetezi Bayern Munich dhidi ya FC Augsburg. Mchezo huo uliishia sare ya mabao 2-2 na pia kusababisha ukosoaji dhidi ya kocha Nico Kovac. Ni vipi Augsburg inayojikuta hivi sasa katika nafasi ya 16 ya msimamo wa ligi na ikiwa na pointi 6 tu baada ya michezo minane imeweza kuwasimamisha mabingwa watetezi, anafafanua hapa mchezaji Stephan Lightsteiner wa Augusburg.
"Nafikiri , tumepambana kuzuwia kwa mikono na miguu leo. Mlinda mlango Koubek alifanya kazi nzuri sana leo. Na pia tuliweza kwa upande wa ulinzi kufanya vizuri. Bila shaka si rahisi dhidi ya Bayern kujilinda hadi mwisho. Ni kweli kwamba walituachia nafasi ya kupumua na hadi mwisho tulijiamini na kupata bao na kupata sare ya mabao 2-2.
Bayer Leverkusen ilishangazwa na Eintracht Frankfurt kwa kipigo cha mabao 3-0 siku ya Ijumaa , na jana Schalke 04 ilishindwa kuchupa hadi nafasi ya kwanza pale walipoduwazwa kwa mabao 2-0 dhidi ya TSG Hoffenheim. Nayo FC Kolon jana imechupa kutoka nafasi ya 17, hadi nafasi ya 15 , baada ya kuikandika SC Paderborn 07 kwa mabao 3-0 nyumbani na kujikusanyia jumla ya pointi 7.
Hata hivyo msuguano kuelekea kileleni mwa msimamo wa ligi ni mkubwa, ambapo timu tisa zina uwezo wa kukalia kiti cha usukani katika mchezo wa 9 wa Bundesliga. Timu 4 zinafungana katika pointi 4, timu 3 zina pointi 15 na timu mbili zina pointi 16, tofauti ikiwa pointi 2 kati ya timu ya tisa Bayer Leverkusen na timu inayoshikilia nafasi ya kwanza Borussia Moenchengladbach yenye pointi 16.