1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MichezoZambia

Timu nne za Afrika zashiriki Kombe la Dunia la Wanawake 2023

19 Julai 2023

Timu nne za Afrika zinashiriki katika Kombe la Dunia la Wanawake mwaka 2023, lakini shauku yao inafifia kutokana na mazingira mabaya ya kazi, malipo yasiyo ya haki na unyanyasaji wa kingono.

Fußball Frauen | Deutschland - Sambia | Barbra Banda
Mshambuliaji nyota wa Zambia, Barbra Banda na Kathrin Hendrich, beki wa UjerumaniPicha: Roland Krivec/DeFodi Images/picture alliance

Kombe la Dunia la Wanawake linaanza Julai 20, huku timu nne za Afrika zikishiriki. Timu hizo ni kutoka Afrika Kusini, Morocco, Zambia, na Nigeria. Hiyo inapaswa kuwa sababu ya kufurahia, lakini miezi kadhaa kabla ya Kombe la Dunia la Wanawake, kumekuwa na kashfa moja baada ya nyingine.

Kumekuwa na timu kususia kwa sababu ya kukosekana mikataba, malipo madogo na viwanja duni. Na kocha wa Zambia ametuhumiwa kwa unyanyasaji wa kingono.

Malipo kidogo

Wiki mbili kabla ya mechi ya ufunguzi, timu ya Afrika Kusini ilisusuia mechi ya maandalizi kwa sababu ya ukosefu wa marupurupu yaliyotolewa na Shirikisho la Soka la Afrika Kusini, SAFA, na hakuna makubaliano ya kimaandishi kuhusu malipo ya Kombe la Dunia.

Timu ya soka ya wanawake ya Nigeria imekumbana na suala kama hilo. Shirikisho la Soka la Nigeria, linazuia marupurupu ya mechi ya wachezaji wake wa Kombe la Dunia la Wanawake waliokataa kufanya mazoezi kwa sababu ya malipo ya mishahara ambayo bado haijalipwa.

Timu ya taifa ya wanawake ya NigeriaPicha: Tobi Adepoju/Shengolpixs/IMAGO

Afrika Kusini na Nigeria, sio tu nchi ambazo zinapambana kuwalipa wachezaji wao. Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na FIFPRO, chama cha wafanyakazi kinachowawakilisha wanasoka wa kulipwa wa kimataifa, ulionesha kuwa asilimia 38 ya wanasoka wanawake wa Shirikisho la Soka Afrika, CAF walisema panahitajika kuwepo na marekebisho makubwa katika malipo yao.

Tofauti ya malipo kutokana na jinsia

Asilimia 29 ya wanasoka wanawake wa kimataifa wamesema hawajapokea malipo yoyote kutoka kwenye timu zao za taifa.

Shirikisho la Soka la Afrika Kusini, SAFA limetangaza malipo sawa kwa wachezaji wote. Zambia na Sierra Leone hadi sasa ndizo nchi pekee za Afrika zinazotekeleza malipo sawa. Timu ya wanaume ya Zambia, haijawahi kamwe kucheza katika Kombe la Dunia.

Tofauti na mashirikisho ya kitaifa, malipo ya Shirikisho la Soka Duniani, FIFA yako wazi. Kila mchezaji anayeshiriki katika hatua ya makundi atalipwa dola 30,000 moja kwa moja kutoka FIFA.

Kwa kawaida pesa hizo zinapelekwa kwenye mashirikisho hayo, na hivyo kusababisha malipo ya mchezaji mmoja kupungua. Hata hivyo, ni tofauti kubwa na michuano ya Kombe la Dunia kwa wanaume ambapo kila taifa lilipokea dola milioni 9 kwa ajili ya kushiriki katika hatua ya makundi.

Mazingira duni ya kazi

Timu ya wanawake ya Afrika Kusini ilisusuia mechi ya mazoezi kwa sababu ya mazingira mabaya ya udongo na nyasi kwenye viwanja, ambayo yangeweza kusababisha majeraha, wiki kadhaa kabla ya kuanza kwa michuano ya Kombe la Dunia la Wanawake.

Wachezaji wa Zambia pia walikumbana na hali kama hiyo ya viwanja duni. Kiungo wa Zambia, Evarine Katongo, amekiambia kituo cha televisheni cha Ujerumani, NTV kwamba viwanja vya mazoezi vilivyo bora zaidi vimetengwa kwa ajili ya timu za wanaume.

Ripoti ya FIFPRO inaonesha kuwa asilimia 26 ya wanasoka wanawake wa CAF, walionyesha kuwa viwanja vyao vinapaswa kufanyiwa marekebisho makubwa.

Unyanyasaji wa kingono

Ripoti ya gazeti la The Gurdian ilidai kuwa kocha mkuu wa Zambia, Bruce Mwape, anachunguzwa na Shirikisho la Soka la Zambia, FAZ, na suala lake limepelekwa FIFA na polisi. Kocha huyo anatuhumiwa kwa unyanyasaji wa kingono.

Timu ya taifa ya wanawake ya MoroccoPicha: Ryan Wilkisky/Sports Inc/empics/picture alliance

Mchezaji mmoja wa timu ya soka ya wanawake wa Zambia ambaye hakutaka kutajwa jina, amesema iwapo kocha anataka kulala na mtu, lazima useme ndiyo. "Ni kawaida kwamba kocha analala na wachezaji kwenye timu yetu," mchezaji huyo aliliambia gatezi moja la Uingereza.

Mkurugenzi wa sheria wa FIFPRO, Roy Vermeer, ameiambia DW kwamba kesi ya Zambia haikuwashangaza. Vermeer amesema hilo ni tatizo la kimuundo katika soka la wanawake ambayo hutokea duniani kote.

Unyanyasaji wa kingono umeripotiwa pia katika timu za Sierre Leone na Gabon. Kuna visa kama hivyo pia vimeripotiwa Marekani, Venezuela, Australia, Haiti na Uhispania. Vermeer anasema katika mashirikisho ya kitaifa mara nyingi hakuna nia ya kuchunguza kesi. Ameiambia DW kuwa kinachohitajika ni kuanzishwa kwa chombo kimoja huru kwa wanasoka ambacho kinachunguza unyanyasaji.

Bado kuna masuala yasiyozingatia haki

Mazingira mabaya ya kazi, malipo yasiyo ya haki na unyanyasaji wa kingono bado yanaendelea kwenye timu za kandanda za wanawake barani Afrika, na pia katika kiwango cha kimataifa. Walakini, katika timu zote za Kiafrika kumekuwa na maboresho, kama malipo sawa.

Soma zaidi: FIFA yazindua vitambaa vya kutetea haki Kombe la Dunia la Wanawake

Kombe la Dunia la Wanawake, huwapa wachezaji nafasi ya kuzungumza kuhusu kutopewa haki yao na kusikilizwa, na kuwatia moyo wanawake wengine kuzungumza. Na kama tunavyoona, wanawake zaidi na zaidi ulimwenguni wanapaza sauti zao.

(DW)