1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AFCON: Timu ya Kongo yaahidi "kuwaburudisha" mashabiki wake

7 Februari 2024

Kocha wa timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Sebastien Desabre amesema anatumai timu yake itatumia mechi hii ya nusu-fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON ili "kuwafariji" wakongomani.

Kandanda | Michuano ya AFCON | Mchezaji wa Kongo Fiston Mayele
Mchezaji wa Kongo Fiston Mayele akiufuata mpira katika mechi dhidi ya Tanzania kwenye Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika-AFCON huko Ivory Coast:24.01.2024 Picha: Fadel SennaAFP/Getty Images

Sebastien Desabre amesema anatarajia kuwa timu hiyo  "itatoa furaha" kwa wakongomani wanaoteseka kutokana na ghasia zinazoendelea mashariki mwa nchi hiyo.

Desabre amewaambia waandishi wa habari mjini Abidjan kwamba mechi ya leo dhidi ya wenyeji Ivory Coast ni maalum, na wanataka watu wanaoteseka huko Kongo wajivunie timu yao ya taifa na kwamba ni kazi yao kuwapa watu furaha na kuwafanya watabasamu.

Timu ya Kongo  inashiriki mechi yake ya kwanza ya nusu fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika tangu mwaka 2015, walipokutana pia na Ivory Coast na kupoteza kwa mabao 3-1.

Kocha huyo raia wa Ufaransa amefanya mabadiliko makubwa katika timu hiyo tangu alipochukua mikoba mwezi Agosti mwaka 2022 baada ya Kongo kupoteza mechi zao mbili za mwanzo za kuwania kufuzu kwenye michuano hiyo.

Wachezaji pia wauangazia mzozo huo

Mshambuliaji wa timu ya Kongo Cedric Bakambu (kushoto) akiwa ana kwa ana na mchezaji wa Zambia Stoppila Sunzu katika mechi ya AFCON: 17.01.2024Picha: Sia Kambou/AFP

Nahodha wa timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Chancel Mbemba na mshambuliaji Cedric Bakambu wameuangazia mzozo unaoendelea mashariki mwa Kongo wakati nchi yao inashiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON.

Bakambu, ambaye amecheza mechi zote hadi sasa na kuisaidia timu hiyo inayojulikana kama "Chui" kufika nusu fainali, ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X kuwa, ulimwengu umepuuza ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Kongo.

Mchezaji huyo ameandika kuwa, kila mtu anaona mauaji yanayofanyika mashariki mwa Kongo ila wamekaa kimya. Ametoa mwito kwa watu kuzungumzia juu ya mzozo wa Kongo kama wanavyotumia nguvu nyingi kuangazia michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika inayoendelea nchini Ivory Coast.

Soma pia: Mechi za nusu fainali za AFCON kutifua vumbia kuanzia Jumatano

Mbemba kwa upande wake, ametumia mtandao wa kijamii wa X kuonyesha mshikamano na wahasiriwa wote mjini Goma. Nahodha huyo wa Kongo amesema anaiombea amani nchi yake.

Eneo la mashariki mwa Kongo limekumbwa na ghasia kwa miongo kadhaa sasa huku zaidi ya makundi 120 yenye silaha yakipigania udhibiti, ardhi na raslimali ya madini katika eneo hilo.

Nigeria na Ivory Coast zapigiwa upatu

Timu ya Ivory Coast ikishangilia ushindi baada ya kuicharaza Senegal katika mechi ya AFCON: 20.01.2024Picha: Themba Hadebe/AP/picture alliance

Katika mechi za leo Jumatano (07.02.2024) za nusu fainali ya michuano ya AFCON, timu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo itachuana na Ivory Coast huku Nigeria ikishuka dimbani na Afrika Kusini.

Soma pia: Nigeria yalenga kubeba taji la AFCON

Nigeria ambayo mchezaji wake nyota Victor Osimhen atakuwa uwanjani leo baada ya kuwepo hofu kwamba huenda angeukosa mchezo huo muhimu kutokana na jeraha.

Licha ya wachambuzi wengi wa soka kusema kuwa Nigeria na wenyeji Ivory Coast wana nafasi kubwa ya kushinda mechi za leo, kipenga cha mwisho ndicho kitaamua ni timu gani zitakazochuana fainali.

(Vyanzo: Mashirika)