1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Timu za England zakabiliwa na mtihani

16 Machi 2026

Klabu za England ziko kwenye shinikizo kubwa Ligi ya Mabingwa baada ya matokeo mabaya ya mkondo wa kwanza. Arsenal pekee inaonekana kuokoa heshima ya Premier League huku vigogo wengine wakipambana kufuta vipigo vizito.

Champions League 2025/26 | Bayer 04 Leverkusen vs. Arsenal FC
Arsenal itakuwa mwenyeji wa Leverkusen ndani ya uwanja wa Emirates.Picha: Marvin Ibo Güngör/GES/picture alliance

Timu za England zinashuka dimbani wiki hii kujaribu kuepuka kuondolewa kabisa katika hatua ya 16-bora ya Ligi ya Mabingwa, huku hadhi ya Ligi Kuu ya England ikiwa mashakani.

Klabu zote sita za England  — idadi kubwa zaidi kuwahi kuwakilishwa na nchi yoyote katika mashindano haya — zilishindwa kushinda mechi zao za mkondo wa kwanza wiki iliyopita,  Arsenal pekee, vinara wa Premier League, wanaoonekana kuwa na nafasi nzuri ya kusonga mbele.

Arsenal wataikaribisha Bayer Leverkusen Jumanne wakiwa sare 1-1, na wanaonekana kuwa wawakilishi wanaoaminika zaidi wa ligi tajiri ya Ulaya katika robo fainali.

Mfululizo wa vipigo vitatu vya mabao matatu — ingawa vyote vilikuwa ugenini dhidi ya wapinzani wenye ubora wa juu — uliwafanya wachambuzi wengi kunukuu kauli maarufu ya Michel Platini kuhusu uchovu wa timu za England: "Simba wakati wa baridi, wana-kondoo ifikapo masika."

Manchester City wataanzia nyuma 3-0 nyumbani dhidi ya Real Madrid.

Chelsea wana deni la mabao 5-2 dhidi ya mabingwa watetezi PSG.

Tottenham wako nyuma 5-2 dhidi ya Atletico Madrid.

Liverpool wanatumai nguvu ya Anfield itawasaidia kufuta kipigo cha 1-0 kutoka Galatasaray.

Newcastle watasafiri kwenda Barcelona wakiwa sare 1-1.

Kabla ya mechi Stamford Bridge, macho yatakuwa kwa wachezaji wa Chelsea kuona kama watafanya tena "huddle” ya pamoja katikati ya uwanja — tukio lililomzunguka mwamuzi Paul Tierney na kuzua kejeli nyingi. Hata Paris, walifanya hivyo mara mbili na wakapigiwa kelele na mashabiki wa PSG.

Katika mechi nyengine

Bodø/Glimt wanaongoza 3-0 dhidi ya Sporting Lisbon. Bayern Munich wanaongoza 6-1 dhidi ya Atalanta.

Mashabiki wa Bodø/Glimt wakiishangilia timu yao wakati wa mechi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Sporting Lisbon.Picha: Martin Ole Wold/Getty Images

Miaka 10 iliyopita, Real Madrid ilimpandisha kocha kutoka ndani ya klabu — Zinedine Zidane — na ikafanikiwa kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa mara tatu mfululizo. Sasa, hali hiyo inajirudia kwa Álvaro Arbeloa, aliyeshinda mtihani wake mkubwa wiki iliyopita dhidi ya Man City.

Fede Valverde aling'ara kwa kufunga hat-trick kipindi cha kwanza licha ya kukosekana kwa nyota waliojeruhiwa Kylian Mbappé na Jude Bellingham. Mbappé anatarajiwa kurejea uwanjani mjini Manchester.

Bodø/Glimt hawapaswi kuogopa uwanja wa José Alvalade wenye viti 52,000, kwani tayari wameshinda kwenye viwanja vikubwa kama Metropolitano (Atletico Madrid) na San Siro (Inter Milan). Ushindi wao dhidi ya Atletico.

Ikiwa Bodø/Glimt watasonga mbele, basi Arsenal au Leverkusen watasafiri hadi uwanja wao mdogo wa Aspmyra viti 8,000.

Real Madrid na Bayern Munich wanaelekea kukutana kwa mara ya 11 katika hatua za mtoano tangu 1992, ingawa hawajawahi kukutana fainali.

Robo fainali nyingine inaweza kuwa kati ya Atletico Madrid dhidi ya Barcelona au Newcastle.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW