Timu za Uingereza zina kibarua kigumu Ulaya
16 Machi 2015Baada ya ushindi wao wa ugenini dhidi ya wapinzani wa Uingereza, Barcelona na Monaco wanapigiwa upatu kufuzu katika nane za mwisho wakati wa mechi za marudiano kesho Jumanne na Jumatano.
Kufuatia kubanduliwa kwa Chelsea, Ligi Kuu ya Premier inakabiliwa na kitisho cha kukosa kushiriki robo fainali, kwa mara ya pili katika miaka mitatu. City itacheza Jumatano uwanjani Camp Nou baada ya kuzabwa na Barca mbili moja katika mechi ya kwanza wakati Arsenal wakihitajika kugeuza magoli matatu kwa moja katika ngome ya Monaco kesho.
Viongozi wa Italia Juventus watakuwa wageni wa Borussia Dortmund Jumatano wakiwa mbele magoli mawili kwa moja, wakati Leverkusen wakisafiri kupambana na mabingwa wa Uhispania Atletico Madrid wakiwa na faida ya goli moja kwa sifuri.
Washindi watajiunga na mabingwa watetezi wa Kombe hilo Real Madrid, mabingwa wa mwaka wa 2013 Bayern Munich, Paris Saint-Germain na Porto katika droo ya robo fainali itakayoandaliwa Ijumaa.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman