Tisa wauawa katika mapigano mpaka wa Somalia na Kenya
25 Januari 2021Somalia inawatuhumu wanajeshi wa Kenya na wapiganaji waliopewa mafunzo na Kenya kwa kuvishambulia vikosi vyake vya shirikisho. Kenya imekanusha kuhusika kwa vyovyote vile katika mapigano hayo.
Mapigano hayo ndiyo tukio la karibuni zaidi linalohusiana na mzozo wa kisiasa katika jimbo la Somalia lenye mamlaka yake ya ndani la Jubaland, ambalo limeutia doa uhusiano wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo ya mashariki mwa Afrika.
Kenya inamuunga mkono rais wa jimbo la Jubaland Ahmed Madobe, ambaye amekuwa katika mkwaruzano na serikali kuu ya Somalia mjini Mogadishu, na anakataa kushiriki katika uchaguzi ambao tayari umecheleweshwa.
"Vikosi vya taifa vya Somalia vilizuwia na kukomesha uvamizi wa alfajiri dhidi ya Bulohawo, uliofanywa na wanajeshi wa Kenya na wanamgambo waasi wa Somalia waliopewa mafunzo na Kenya, waliojaribu kuchukua udhibiti wa mji huo," waziri wa habari Osman Abukar Dube aliuambia mkutano wa habari mjini Mogadishu.
"Vikosi vya Somalia viliwakamata wanamgambo waasi 100 waliopewa mafunzo na Kenya wakati wa mapigano, na wanazuwiliwa katika eneo salama."
Waziri huyo aliituhumu Kenya na wanamgambo hao kwa "kuyashambulia kwa mabomu makaazi ya watu na kuuawa watoto watano na mama yao katika moja ya mashambulizi hayo."
Kamanda wa kijeshi mjini Bulohawo, Kanali Mohamed Abdulle, alisema wanajeshi watatu waliuawa. Lakini idadi jumla ya vifo haikuweza kuthibitishwa na vyanzo huru.
Soma pia: Somalia: Watu watano wauawa kwenye shambulio la kujitoa mhanga
Waziri wa usalama wa ndani wa Kenya Fred Matiangi alisema mapigano hayo yalikuwa yanahusiana na mzozo wa "ndani" wa Somalia. "Hatushiriki katika mzozo huo na hakuna kati ya wanajeshi wetu alievuka mpaka kuingia Somalia," alisema.
Ahmednur Yusf, mkaazi wa Bulahawo, aliliambia shirika la habari la AFP kwamba aliona "miili ya watu wanane, watoto kutoka familia moja, ambao nyumba yao ilipigwa na kombora".
"Niliona wafungwa kadhaa wa kivita waliotekwa na vikosi vya Somalia kutoka wanajeshi wa Jubaland, walikuwa wamepanga foreni na kupelekwa katika kambi ya kijeshi nje ya mji huo," alisema.
Ali Roba, gavana wa kaunti ya Mandera kwenye upande Kenya wa mpaka, alisema katika taarifa kwamba watu 12 walilazwa hospitali wakiwa na majeraha kutokana na risasi zilizokwenda kombo, na kombora lililopiga nyumba katika mji huo.
Kenya inaitazama Jubaland -- ambayo ni sehemu ya Somalia yenye utulivu na ustawi kiasi, ambako ina wanajeshi wake wengi -- kama kizuwizi kati yake na wapiganaji wa Al-Shabaab ambao wamefanya mashambulizi kadhaa mabaya kwenye mipaka yake,
Soma pia: Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Somalia na Kenya mashakani
Juni mwaka uliyopita Mogadishu ilimtambua rasmi Madobe kama kiongozi wa Jubaland kufuatia uchaguzi uliobishaniwa Agosti 2019.
Hata hivyo, vikosi vya Somali havijaondoka jimboni humo kama ilivyoahidiwa, na Jubaland inakataa kushiriki uchaguzi wa kitaifa uliopaswa kufanyika mwezi Februari, lakini umekuwa ukikabiliwa na ucheleweshaji wa mara kwa mara.
Mnamo mwezi Desemba, Somalia ilivunja uhusiano wa kidiplomasia na Kenya kwa tuhuma za "kuingilia" siasa za ndani za taifa hilo.