Tishio la ugaidi laongezeka barani Afrika
3 Julai 2018Makundi ya itikadi kali yanasonga mbele barani Afrika na ndiyo sababu kwenye mkutano wa viongozi wa Umoja wa Afrika suala la usalama limepewa kipaumbele. Wiki iliyopita waziri wa mambo ya nje wa Morocco, Nasser Bourita, alitahadharisha juu ya hatari hiyo.
Nasser Bourita alitanabahisha kwamba wapo wapiganaji wapatao 10,000 wenye itikadi kali ya Kiislamu na hasa wapiganaji wa mtandao wa kigaidi wa al-Qaida pamoja na wale wanaorejea kutoka kwenye maeneo yaliyokuwa yanadhibtiwa na magaidi wanaojiita Dola la Kiislamu - IS, nchini Syria na Irak.
Waziri huyo wa mambo ya nje wa Morocco amesema katika mahojiano na DW kwamba idadi aliyoitaja ya magaidi hao siyo ya kutia chumvi kwa sababu inapasa kuyatia katika hesabu makundi ya magaidi ya al-Shabaab wa Somalia na Boko Haram wa Nigeria. Waziri huyo amesema mkakati thabiti dhidi ya magaidi wenye itikadi kali ya Kiislamu unahitajika barani Afrika.
Nchi za kaskazini mwa Afrika zinapaswa kuimarisha harakati dhidi ya Waislamu wenye itikadi kali katika ngazi zote ikiwa ni pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa pamoja na kundi la nchi tano za ukanda wa Sahel zinazokabiliana na magaidi katika eneo lao, maarufu kama G5.
Mnamo mwaka 2014, kundi la nchi hizo lilizinduliwa kwa madhumuni ya kupambana na magaidi. Nchi hizo ni pamoja na Mauritania, Mali, Niger, Burkina Faso na Chad. Ni katika eneo hilo ambako makundi ya magaidi yaliwashambulia wanajeshi wiki iliyopita.
Je, ni kweli kwamba wapo wapiganaji wa kigaidi 10,000? Mwandishi habari na wa vitabu, Marc Engelhardt, amesema katika mahojiano na DW kwamba hakuna mahala ambapo watu hao wamesajiliwa. Hata hivyo, anaamini kwamba idadi hiyo ya watu 10,000 ni kubwa mno. Mwandishi huyo amesema ni jambo la kutia wasiwasi kwamba idadi ndogo tu ya wapiganaji hao wanaweza kuwa tishio kubwa kwa nchi kama Mali na kuigeuza kuwa mateka.
Mwandishi huyo ametahadharisha kwamba nchi nyingi za Afrika zinazidi kulengwa na magaidi na siyo tu katika maeneo ya migogoro, kama vile ukanda wa Sahel, kaskazini mwa Afrika, Somalia na Nigeria. Magaidi wenye itikadi ya Kiislamu pia wameingia katika nchi ambako hatari hiyo ilikuwa haijulikani kama katika nchi za Burkina Faso, Ivory Coast na Msumbiji.
Engelhardt anasema Uislamu unatumiwa kwa sababu za kigaidi. Lakini hasa wale wanaopanga na kuongoza mashambulio ya kigaidi wanawania kupata mamlaka na faida. Wanaitumia dini ya Kiislamu kama njia ya kufikia kwenye shabaha zao. Hata hivyo, pia inapasa kutilia maanani kwamba, viongozi wa magaidi wanaheshimiwa na kuenziwa na watu wanaoishi pembezoni mwa jamii, yaani maskini katika maeneo masikini.Viongozi wa kidini wanaohubiri itikadi kali kali na wafuasi wao wanapokelewa kwa mikono miwili na makundi ya kigaidi.
Lengo la nchi za Umoja wa Afrika ni kuitatua migogoro yote ya kivita barani humo hadi kufikia mwaka wa 2020 lakini baadhi ya viongozi wanahoji kwamba muda wa miezi 18 uliobakia ni mfupi. Hata hivyo mwakilishi wa Umoja wa Afrika nchini Mali na katika ukanda wa Sahel amesema mapambano dhidi ya magaidi yataendelea kuwa changamoto itakayopewa kipaumbele barani Afrika.
Mwandishi: Zainab Aziz/ Antonio Cascais
Mhariri: Mohammed Khelef