1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TLS yakosoa visa dhidi ya Wamaasai walioko Ngorongoro

20 Agosti 2024

Chama cha wanasheria nchini Tanzania, Tanganyika Law Society kimesema kinachoendelea kwa wamasaai walioko katika eneo la hifadhi ya taifa Ngorongoro kinalenga kuwaondoa, kuwanyima huduma muhimu na ukiukwaji wa sheria.

Tanzania | Maasai walioko Ngorongoro
Baadhi ya wakazi wa jamii ya Wamasai walipokusanyika katika eneo la Ngorongoro Tanzania kupinga vikwazo vya serikali kutumia ardhi hiyo Agosti 9, 2023Picha: Deinis Olushangai

Tamko la chama hicho lifuatia maandamano ya amani yaliyofanywa na wamasai hao wanapinga hatua za mamlaka nchini humo kusitisha huduma muhimu ikiwemo shule na hospitali.

Huku kikitoa kauli ya kupinga vikali hatua zote zinazochukuliwa na mamlaka juu ya wakazi hao wanaotajwa kuwa wa asili katika eno hilo, TLS pia imetangaza kuunda kamati ya wataalamu wa sheria kwa ajili ya kutathmini hali jumla ya mambo katika eneo hilo.

Soma pia: HRW: Tanzania yawafurusha maelfu ya Wamaasai

Rais wa chama hicho aliyeingia katika nafasi hiyo hivi karibuni, wakilli Boniface Mwabukusi amesema kamati hiyo imepewa muda siku 30 kuchunguza na kutathimini yale yote yanayoendelea katika eneo hilo na inaanza kutekeleza majukumu yake Agosti 21.

Serikali imekuwa ikiratibu hatua za kuwaondoa wakazi hao

Serikali imekuwa ikiratibu mchakato wa kuwaondoa wakazi hao, ambao inasisitiza kuwa umekuwa ukifanyika kwa hiari na kwenda kuwatafutia makazi mapya katika eneo jipya la Msomera lililopo mkoani Tanga.

Makazi ya Wamaasai yaliyojengwa katika Hifadhi ya Ngoorongoro kama picha ilivyoonyesha Januari 29, 2024Picha: Hua Hongli/picture alliance

Hata hivyo, hatua hiyo bado imekuwa ikiandamwa na ukosoaji mkubwa kutoka kwa baadhi ya makundi, na hivi karibuni kabisa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC) lilisema kutowasikiliza Wamaasai wanaioshi katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ni kuwanyima haki zao.

Akizungumzia suala hilo, Katibu wa TEC Padri Charles Kitima alihoji hatua za mamlaka kueleza wale wanataka kubaki katika eneo hilo wanafanya hivyo kwa hiari yao huku wakinyimwa haki zao za msingi ni ukiukwaji wa haki za binadamu.

Ripoti kutoka eneo la Ngororongoro zinasema Wamasai wamekuwa wakikusanyika na kutoa matamko ya kulaani kunyimwa huduma muhimu wakisema pamoja na hatua hiyo wataendelea kusalia katika eneo.

Baada ya familia kadhaa kuamua kuanzisha makazi mapya huko Msomera, eneo hilo sasa limesaliwa na kata 11 yenye vijiji 25. 

Sikiliza zaidi: 

Kamatakamata ya raia Ngorongoro

This browser does not support the audio element.