Tofauti kati ya Ujerumani na Marekani yazidi kutokota
30 Mei 2017Rais wa Marekani Donald Trump kwa mara nyingine amesema kuwa sera ya Ujerumani kuhusu biashara pamoja na matumizi ya fedha za kijeshi ni mbaya mno kwa Marekani. Matamshi ya Trump yamekuja saa chache tu baada ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kusema kuwa mahusiano kati ya nchi hizo yamebadilika pakubwa kufuatia kukosekana kwa maafikiano wakati wa mkutano wa nchi saba zilizoendelea zaidi kiviwanda wiki iliopita.
"Tunao upungufu mkubwa wa kibiashara na Ujerumani. Isitoshe wanalipa kiwango cha chini mno kuliko kile wanachopaswa kulipa kwa matumizi ya jeshi la Jumuiya ya Kujihami ya NATO. Hiyo ni mbaya sana kwa Marekani. Hilo litabadilika." Huo ndio ujumbe ambao Rais Donald Trump aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter, kama jibu kwa maneno ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel hapo jana dhidi yake, ambapo Merkel alizungumzia athari ya msimamo wa utawala wa Marekani kwa uhusiano wake na Ulaya.
Mara kwa mara, Trump ameitaka Ujerumani kutimiza kiwango cha fedha kwa jeshi la Jumuiya ya kujihami ya NATO ambayo ni asilimia 2 ya pato jumla la nchi hiyo. Isitoshe mara kwa mara Trump hutaja sera ya Merkel ya kuwafungulia milango wakimbizi kuwa kosa linaloweza kusababisha janga.
Mvutano kati ya Marekani na Ujerumani ulianza wakati wa mkutano wa kilele wa wakuu wa nchi 7 zilizoendelea sana kiviwanda G-7, uliofanyika Taormina Italia wikendi iliyopita, pale Trump alipotangaza kuwa anahitaji muda zaidi kuamua ikiwa Marekani itajiondoa au itaheshimu mkataba wa Paris kuhusu mabadiliko ya tabia nchi. Mkataba huo unataka nchi kupunguza utoaji wa gesi chafu zinazosababisha ongezeko la joto duniani.
Aidha, uhusiano kati ya Marekani na Ujerumani umezongwa na matatizo kufuatia ukosoaji wa mara kwa mara kutoka kwa Trump kuhusu upungufu wa biashara za Marekani nchini Ujerumani ikilinganishwa na za Ujerumani nchini Marekani, na hata Trump kutishia kuwa atazitoza kampuni za magari za Ujerumani kodi za juu kwa kuuza magari yaliyotengenezwa kwingine ndani ya Marekani.
Baadaye akiwahutubia waandishi wa habari mjini Berlin, Kansela Merkel alisema kuwa uhusiano wa kidiplomasia na Marekani ni muhimu lakini tofauti kuhusu masuala makuu kama mabadiliko ya tabia nchi inaashiria kuwa Ulaya inahitaji kujitegemea kivyake.
Baadhi ya wanasiasa wakuu wa Ujerumani nao wamejiingiza kwenye mvutano huo. Waziri wa mambo ya nje Sigmer Gabriel ambaye pia ni naibu wa Kansela ameitaka Ujerumani kupinga sera za utawala wa Trump, na wasiofanya hivyo watakuwa wanafanya makosa. Ameliambia gazeti la nchini Ujerumani la Rheinische Post na kuongeza kuwa wale wanaochangia mabadiliko ya tabia nchi wakati wanatoa kiwango cha chini cha fedha kuhifadhi mazingira, wanaouza silaha nyingi kwa nchi zinazokumbwa na mizozo na wasiokuwa na nia ya kusuluhisha migogoro ya kidini kwa njia ya diplomasia wanahatarisha amani ya Ulaya.
Kiongozi wa chama cha Social Democratic SDP Martin Schulz atakayeshindana na bibi Merkel katika uchaguzi wa Ujerumani mwezi septemba, naye amesema kuwa jambo muhimu kwa sasa ni kumpinga Trump kwa kila kitu wanachokisimamia.
Mwandishi: John Juma/DPAE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman