Katiba mpya Togo: Wabunge sasa kumchagua Rais
27 Machi 2024Kulingana na katiba hiyo mpya wabunge ndio watakuwa na jukumu la kumchagua rais ambaye atahudumu kwenye wadhfa huo kwa muhula mmoja wa miaka sita. Hatua hiyo inamaanisha kwamba sasa wananchi sio watakaokuwa wanamchagua rais kwa njia ya kupiga kura.
Soma Pia: Kiongozi wa upinzani atiwa mbaroni Togo
Mabadiliko hayo yamefanyika mwezi mmoja kabla ya uchaguzi wa bunge nchini Togo lakini bado haijajulikana lini mabadiliko hayo yataanza kutekelezwa baada ya kupitishwa kwa kura 89. Kulingana na katiba ya sasa rais anaweza kutumikia mihula miwili ya miaka mitano mitano.
Mabadiliko hayo ya katiba yalipendekezwa na kundi la wabunge walio wengi kutoka chama kinachotawala cha Union for the Republic (UNIR).
Chini ya katiba hiyo mpya, ambayo haizingatii muda ambao tayari rais Faure Gnassingbe ameutumia ofisini,kiongozi huyo sasa anaweza kubaki madarakani hadi mwaka 2031 iwapo bunge litamchagua tena mwaka ujao wa 2025.
Upo uwezekano mkubwa kwa sababu chama chake kinadhibiti Bunge kwa wingi wa viti 89 kati ya jumla ya viti 91. Katiba hiyo mpya pia inatoa nafasi yakuwepo kiongozi wa baraza la mawaziri atakayekuwa na mamlaka kamili ya kusimamia shughuli za serikali.
Soma Pia: Hali nchini Togo bado ya wasiwasi.
Faure Gnassingbe alichaguliwa mnamo mwaka 2020 katika uchaguzi uliosusiwa na upinzani. Wapinzani ambao hawawakilishwi vyema katika bunge la kitaifa nchini Togo waliushutumu uchaguzi huo kwa kuwa na dosari nyingi.
Nchi nyingine nyingi za Afrika, ikiwa ni pamoja na Jamhuri ya Afrika ya Kati, Rwanda, Jamhuri ya Kongo, Ivory Coast na Guinea zimefanya mabadiliko ya kikatiba na mengine ya kisheria katika miaka ya hivi karibuni ya kuruhusu marais wao kuongeza muda wa kubakia madarakani.
Soma Pia: LOME Rais mpya wa Togo, Faure Gnassingbe, ashindwa kujikwamua kutokana na lawama zinazomkabili.
Wakati huo huo kanda za Afrika Magharibi na Kati zikiwa zimeshuhudia mara nane mapinduzi ya kijeshi katika muda wa miaka mitatu iliyopita.
Vyanzo:RTRE/AFP