TOKYO: Marekani yatangaza Korea Kaskazini imekubali kurejea kwenye mashauriano ya pande sita.
20 Januari 2007Mjumbe wa Marekani kuhusu mradi wa nyuklia wa Korea Kaskazini, Christopher Hill, amesema serikali hiyo imekubali kurejea haraka iwezekanavyo kwenye mashauriano ya pande sita kuhusu mradi wake wa silaha za kinyuklia.
Christopher Hill alikuwa akizungumza baada ya mashauriano kati yake na mjumbe wa Japan mjini Tokyo, kituo chake cha pili cha ziara ya mataifa ya Eshia.
Mjumbe huyo wa Marekani alisema mashauriano ya hivi karibuni mjini Berlin yaliweka msingi mzuri wa mkutano wa pande sita utakaoandaliwa nchini China.
Baada ya mkutano wa Berlin, Korea Kaskazini ilisema ilikuwa imeafikiana kwa namna fulani na Marekani.
Mazungumzo ya pande sita yalirejewa mwezi Disemba mwaka uliopita baada ya kusitishwa kwa muda wa mwaka mmoja.
Korea Kaskazini ilitumia muda huo kufanya jaribio lake la kwanza la bomu la kinyuklia.