TOKYO : Wajapani wapiga kura katika uchaguzi wa bunge
29 Julai 2007Wajapani leo wanapiga kura katika uchaguzi wa baraza la juu la bunge ambao unatabiriwa kutowa pigo kubwa kwa Waziri Mkuu Shinzo Abe.
Wachambuzi wa mambo wanasema kwamba Abe huenda akalazimika kujiuzulu iwapo chama chake tawala cha Liberal Demokratik kitapoteza udhibiti wa baraza hilo la juu la bunge juu ya kwamba kinaendelea kuwa na viti vingi kwenye baraza la chini la bunge ambalo ndilo lenye kumchaguwa waziri mkuu.
Umashuhuri wa Abe umepunguwa kutokana na kashfa kadhaa ikiwa ni pamoja na kusimamia vibaya mfumo wa pensheni malipo ya uzeeni ambapo anasema yeye na baraza lake la mawaziri watatuwa matatizo yote ya pansheni kwa kuyakinisha ushahidi wote ili kwamba kila mtu apatiwe malipo ya pensheni yalio sahihi.
Abe mwenye umri wa miaka 52 amekuwa waziri mkuu miezi 10 iliopita wakati Junichiro Koizumi alipojiuzulu na mara kwa mara amesema kwamba ashinde au ashindwe katika uchaguzi huu wa leo ambao ni mtihani wake wa kwanza wa uchaguzi tokea aingie madarakani hatojiuzulu.