Tokyo. Wanamuzi maarufu duniani wanashiriki katika matamasha duniani kote katika kutoa mbinyo kwa wanasiasa kuisaidia zaidi Afrika kuondokana na umasikini.
2 Julai 2005Wanamuziki maarufu wa kimataifa wamepanda katika majukwaa mbali mbali katika matamasha yanayolenga katika kutoa mbinyo kwa wanasiasa wafanye juhudi zaidi katika kupambana na umasikini katika bara la Afrika.
Matamasha hayo manane yanafanyika katika miji 10 mikubwa hapa duniani. Matamasha hayo ya muziki yanafanyika siku chache tu kabla ya mkutano wa viongozi wa kundi la G8, nchi zenye utajiri mkubwa wa viwanda huko Scotland.
Waziri mkuu wa Uingereza Bwana Tony Blair ameliweka suala la kupambana na umasikini katika bara la Afrika kuwa katika agenda ya juu katika mkutano huo wa G8.
Mwanamuziki wa Ireland Bob Geldof ndie aliyetayarisha matamasha hayo manane. Pia ndie aliyetayarisha tamasha la muziki kwa ajili ya kuisaidia Ethiopia miaka 20 iliyopita.
Mamia kwa maelfu ya watu wanatarajiwa kuhudhuria tamasha litakalofanyika nchini Ujerumani katika mji wa Berlin katika lango la Brandenburg.