1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Toni Kroos arudisha shangwe Ujerumani

26 Machi 2024

Akiwa na Kombe la Dunia na mataji mengi ya Bundesliga, La Liga na Ligi ya Mabingwa, Toni Kroos ni miongoni mwa wanasoka waliopambwa zaidi wakati wote. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 34 amerejea kuichezea Ujerumani.

Kandanda| Ujerumani - Ufaransa
Mchezaji Toni Kroos akiwa katika mechi ya kimataifa ya Ujerumani.Picha: Alexander Hassenstein/Getty Images

Ujerumani imekuwa na matokeo magumu katika miaka ya hivi karibuni: kutoka kwa mashindano,  kwa makocha na wachezaji wao walioshinda Kombe la Dunia la 2014. Lakini kurejea kwa mmoja wa wachezaji hao, Toni Kroos, ni miongoni mwa dalili za matumaini mapya kwa waandaji wa Euro 2024.

Soma pia: Kroos ndiye mchezaji bora Ujerumani

Kroos alirejea katika timu ya taifa ya Ujerumani miaka mitatu baada ya kuacha kucheza mechi ya kimataifa kufuatia kuondolewa kwa Ujerumani na England katika Euro 2020 (iliyochezwa 2021).

Athari ya kurudi kwake ilijitokeza baada ya kuachia pasi ndefu ambapo Florian Wirtz aliifungia Ujerumani bao la haraka zaidi la kimataifa baada ya sekunde saba za ushindi wa 2-0 dhidi ya Ufaransa.

Baada ya mechi kiungo huyo wa Real Madrid alisema, "Tunaweza kuridhika sana. Tumepiga hatua nzuri na muhimu mbele. Ilikuwa ni nafasi ya kupata hisia nzuri kuelekea kwenye michuano ya Ulaya.”

 

Kukimbizana na muda

Wachezaji wa timu ya taifa ya Ujerumani Toni Kroos na Kai Haverts wakiwa katika mechi ya kirafiki.Picha: Christian Charisius/dpa/picture alliance

Ni muda umepita tangu timu ya taifa ya Ujerumani ya wanaume kuwa na hisia hizo nzuri. Julian Nagelsmann alichukua nafasi ya ukocha Septemba mwaka jana baada ya matokeo kushuka na kushuhudia Hansi Flick akifukuzwa chini ya miaka miwili baada ya kurithi mikoba ya kocha wa muda mrefu Joachim Löw.

Löw aliyeshinda Kombe la Dunia alijaribu kurejesha viwango vya Ujerumani kwa kuwajumuisha kikosini Thomas Müller na Mats Hummels kabla ya Euro 2020, badala yake timu ilifanya vibaya. Ingawa bado ni mapema kubashiri muelekeo wa Nagelsmann kumjumuisha Kroos kwa sasa hatua hiyo imeonekana kuwa na matunda.

"Toni Kroos alicheza vizuri sana," alisema Nagelsmann baada ya mechi. "Aliweka kasi na kufanya kazi kwa bidii sana. Anawapa wachezaji wengine kujiamini sana."

Ingawa Kroos alifanya vyema, mechi hiyo pia ilikuwa muhimu kwa wachezaji wengine kadhaa wa Ujerumani ambao bado wanajaribu kuweka alama zao, kwa viwango tofauti, kabla ya mechi ya ufunguzi ya Euro 2024 dhidi ya Scotland mnamo Juni 14 huko Munich.

Wachezaji wapya

Kocha wa timu ya taifa ya kandanda wa Ujerumani Julian Nagelsmann akitoa maelekezo kwa kikosi chake.Picha: BEAUTIFUL SPORTS/Wunderl/IMAGO

Maxi Mittelstädt alivutia kama mmoja wa wachezaji watatu walianza vyema katika kuwakilisha taifa, Huku Florian Wirtz na Kai Havertz, wa Bayer Leverkusen, wote wako katika fomu nzuri kwa wakati ufaao.

"Ninapomwona Maxi Mittelstädt, jinsi alivyocheza kwa utulivu katika mechi yake ya kwanza ya kimataifa, hiyo inashangaza kabisa," alisema Kroos kuhusu mchezaji huyo mpya katika nafasi ya beki wa kushoto.

Kwa Havertz, ambaye pia alikuwa amefunga katika mechi zake nne zilizopita za Premier League akiwa na Arsenal, mchezo huu ulionyesha mabadiliko baada ya matokeo mchanganyiko wakati Ujerumani ikijiandaa kwa michuano ya Euro kwa mfululizo wa mechi za kirafiki.

"Ilikuwa mechi ya kufurahisha sana," kijana huyo wa miaka 24 alisema. "Tulidhibiti mechi katika kipindi cha pili. Ni muhimu sana kwamba kila mchezaji ajue jukumu lake kabla ya mashindano kama haya."

Kwa muda, majukumu ndani ya kikosi cha Ujerumani yamekuwa hayaeleweki kwa kiasi fulani. Nagelsmann, Flick na hata Löw wamelazimika kuchukua wachezaji wapya wenye vipaji na kuwaacha nje wale waliotangulia.

Washabuliaji watatu; taswira ya siku zijazo

Wachezaji wa timu ya taifa ya kandanda wa Ujerumani wakisherehekea bao la Florian Wirtz katika mechi ya kirafiki dhidi ya Ufaransa.Picha: Christian Charisius/dpa/picture alliance

Wirtz, Havertz na Jamal Musiala wachezaji watatu wachanga, wenye vipaji na walio katika kiwango bora na Kroos akiongeza uwepo wake wa utulivu na wa hali ya juu katika safu ya kiungo, kuna dalili za mapema kwamba mambo yanaanza kuwa sawa Ujerumani.

"Huo ulikuwa mmoja wa michezo bora zaidi ambayo tumecheza katika miaka ya hivi karibuni," alisema Rudi Völler, mkurugenzi wa michezo wa Chama cha Soka cha Ujerumani (DFB). "Ushindi huu ulistahili. Tulijiamini katika kipindi cha pili. Kurudi kwa Toni Kroos kulikuwa muhimu, alifanya kazi ya ajabu tangu mwanzo."

Ingawa ulikuwa mwanzo wa haraka na mpya dhidi ya Ufaransa, Kroos na Nagelsmann watajua iwapo utakuwa na maana ikiwa utaendelezwa.

 

https://p.dw.com/p/4e40w