Touadera: Je, ni mtu wa amani ama "Rais Wagner"?
8 Agosti 2023Faustine-Archange Touadera, anaetazamiwa kuwania muhula wa tatu kama Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati baada ya wapiga kura kupitisha kwa wingi rasimu ya katiba mpya, anajinasibu kama gundi inayowaunganisha watu katika mojawapo ya nchi zenye machafuko zaidi duniani.
Hata hivyo, wakosoaji wake wanamuita Touadera kama "Rais Wagner" kutokana na utegemezi wake kwa Urusi na kundi la mamluki la Wagner.
Kila wakati anaposafiri, Touadera hukumbushwa juu ya changamoto kubwa inayomkabili katika taifa hilo lililokumbwa na umaskini na kusambaratishwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa zaidi ya muongo mmoja.
Soma pia: Mtuhumiwa wa ujasusi CAR aruhusiwa kurejea Ufaransa
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa na kundi la mamluki la Urusi la Wagner wanamsindikiza Touadera kila anapokwenda, na vikosi hivyo viwili vimemsaidia kiongozi huyo kupambana na waasi.
Touadera mwenye umri wa miaka 66, waziri mkuu wa zamani mwenye historia ya kitaaluma, alishinda muhula wa kwanza katika uchaguzi wa mwaka 2016, wa kwanza kufanyika baada ya kutokea mapinduzi na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyozuka miaka mitatu nyuma.
Wakosoaji wa Touadera wamempa jina la "Rais Wagner"
Matumaini ya awali kuhusu uongozi wake yalififia baada ya makubaliano yenye utata na wababe wa kivita kwa lengo la kuleta amani nchini humo. Pia ushindi wake katika uchaguzi wa mwaka 2021 haukupokewa kwa shangwe.
Wakosoaji sasa wanamuita "Rais Wagner,” wakiashiria utegemezi wake kwa Urusi na kundi la mamluki la Wagner, na kusema Touadera anang'ang'ania kusalia madarakani maisha yake yote.
Soma pia:Afrika ya Kati yaidhinisha rasimu ya katiba mpya
Wakati wapiga kura wakipitisha kwa wingi rasimu ya katiba mpya ambayo inaondoa kikomo cha mihula miwili ya marais na kuongeza muda wa kukaa madarakani kutoka miaka mitano hadi saba, utawala wa Touadera unaweza kuendelea hadi mwaka 2033.
Ukosoaji juu ya ushindi wake wenye utata wa mwaka 2016 ulizimwa wakati huo. Wengi waliuona uchaguzi huo licha ya kukumbwa na dosari, kama kafara kwa ajili ya kupatikana utulivu nchini humo.
Wafuasi wake wanamchukulia kama mchapakazi
Katika kipindi cha baada ya uchaguzi huo, Touadera alijenga taswira kama kiongozi mchapakazi na asiyependa makuu.
Wafuasi wake walimchukulia kuwa mtu mnyenyekevu sana.
Hata hivyo wapinzani wake wanamuona kama kiongozi wa "serikali dhalimu” na iliyosheheni ufisadi unaoiandama nchi hiyo kwa miongo kadhaa.
Wengine wanasema kuwa, kiongozi huyo alirubuniwa na makundi ya wanamgambo ambayo kwa wakati mmoja, walikuwa wamedhibiti zaidi ya theluthi mbili ya nchi hiyo, wakiwashambulia raia na jeshi, na kupigania utajiri wa madini.
Touadera alifikia makubaliano ya amani na makundi 14 yenye silaha mnamo Februari mwaka 2019, na kuwajumuisha wababe wa kivita serikalini kama sehemu ya wanamgambo hao kuweka chini silaha.
Makubaliano hayo yaliwatenga watu wengi ambao walikuwa wakiteseka mikononi mwa wanamgambo hao.
Mataifa ya Magharibi, Shirika la Umoja wa Mataifa na mashirika yasio ya kiserikali yameeleza kuwa Touadera alichukua maamuzi hayo ili kujinusuru kisiasa na kwa kiasi fulani, kuleta utulivu katika sekta ya madini nchini humo.
Soma pia: Kura zahisabiwa Jamhuri ya Afrika ya Kati
Makampuni ya Urusi yanayohusishwa na Wagner yamejipatia utajiri mkubwa kupitia ruzuku ya madini licha ya Jamhuri ya Afrika ya Kati kutegemea misaada ya kimataifa.
Kuingilia kati kwa mamluki wa Wagner mwaka 2020 kulilisaidia jeshi la serikali katika mapambano yake na waasi ambao walikuwa wameuzingira mji mkuu Bangui na kutishia kuipindua serikali ya Touadera.
Jamhuri ya Afrika ya Kati yakumbwa na umaskini
Uhusiano kati ya Touadera na Ufaransa, iliyoitawala nchi hiyo wakati wa enzi za ukolononi pia umeyumba. Ufaransa iliingia kati kijeshi mwaka 2013 na kusaidia kuzuia umwagaji damu wa raia.
Wakati huo, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema kuwa Touadera amekuwa "mateka” wa wale aliowaita "wanyanyasaji” wa mamluki wa Urusi.
Touadera alishinda uchaguzi tena mwaka 2021 kwa kupata asilimia 53.16 ya kura japo asilimia 35.25 tu ya watu ndio waliojitokeza kushiriki uchaguzi huo.
Wapiga kura wengi hawakuweza kupiga kura katika maeneo yaliyo nje ya udhibiti wa serikali.
Kwa wafuasi na wapambe wanaomuunga mkono, Touadera amechukua moja kati ya vibarua visivyokuwa na fadhila.
Alichukua usukani wa nchi ambayo mara kwa mara inashika nafasi ya chini katika ripoti ya maendeleo ya binadamu ya Umoja wa Mataifa, ambayo hutumiwa kama alama ya ustawi wa nchi.