1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TPLA yazilaumu Iran, Uturuki na UAE kwa kuchochea vita.

Zainab Aziz Mhariri: Tatu Karema
19 Desemba 2021

Kiongozi wa kundi la TPLA katika jimbo la Tigray amezilaumu Iran, Uturuki na Umoja wa Falme za Kiarabu kwa kuchochea vita nchini Ethiopia.

Äthiopien Tigray Debretsion Gebremichael
Picha: Eduardo Soteras/Getty Images

Kiongozi wa jimbo la Tigray, Debretsion Gebremichael amesema mgogoro wa Ethiopia unazidishwa na kujiingiza kwa nchi za nje, huku akizilaumu nchi za Iran, Uturuki na Umoja wa Falme za Kiarabu kwa kuukoleza moto mgogoro wa nchi hiyo kwa kuipa serikali kuu ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Ahmed Abiy misaada ya kijeshi na kifedha.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abbiy AhmedPicha: Minasse Wondimu Hailu/AA/picture alliance

Gebremichael aliyasema hayo katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Tigray. Amesema majeshi ya kigeni na ya ndani yalitenda ukatili wakati wa vita katika miezi ya hivi karibuni ambapo ndege zisizo na rubani zilishambulia maeneo mbalimbali katika mkoa wa Tigray.

Kwa upande wake serikali kuu ya Ethiopia imewalaumu wapiganaji wa Tigray kwa kuwaua raia na kuharibu miundombinu katika maeneo yaliyokuwa chini ya udhibiti wao.

Mapigano kati ya kundi la TPLF na majeshi ya serikali kuu ya Ethiopia yameendelea kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa na yamesababisha vifo vya maelfu ya watu. Mashirika ya misaada yamesema mamilioni ya watu wanahitaji msaada wa haraka.

Kushoto: Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed. Kulia: Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan.Picha: Serhat Cagdas/AA/picture alliance

Kauli hiyo ya kiongozi wa jimbo la Tigray ameitoa wakati ambapo Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed anahudhuria mkutano wa tatu wa wakuu wa nchi na serikali kati ya Uturuki na viongozi wa bara la Afrika mjini Istanbul.

Leo Jumapili, Waziri wa Ulinzi wa Ethiopia Abraham Belay amekutana na waziri mwenzake wa Uturuki Hulusi Akar na walizungumzia juu ya mafanikio ya Uturuki katika teknolojia ya ulinzi.

Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan ameuambia mkutano wa kilele kati ya Uturuki na Afrika mjini Istanbul kwamba nchi yake itaimarisha zaidi uhusiano wa kibiashara na bara la Afrika. Amesema serikali yake inapanga kuongeza biashara kufikia dola bilioni 75 kwa mwaka. Mwaka huu Uturuki ilifanya biashara na bara la Afrika kufikia kiasi cha dola bilioni 30.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Mevlut CavusogluPicha: AFP via Getty Images

Uturuki ina balozi 43 kati ya jumla ya nchi 54 za Afrika na inaendesha mipango mikubwa ya misaada ya kijamii, nishati, miradi ya ulinzi na miundombinu.

Waziri wa Mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu amesema jumla ya viongozi 16 na mawaziri 102 kutoka Afrika walihudhuria mkutano huo wa tatu wa kilele, wa mjini Istanbul uliofanyika kutoka tarehe 16.12.2021 na kumalizika 18.12.2021.

Chanzo: dpa