1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TPLF yasema iko tayari kwa mazungumzo ya amani

12 Septemba 2022

Wapiganaji kwenye jimbo la Tigray nchini Ethiopia wamesema wako tayari kusitisha mapigano na kuridhia mchakato wa kusaka amani chini ya Umoja wa Afrika.

Äthiopien | Kämpfer der Tigray People's Liberation Front
Picha: Ben Curtis/AP Photo/picture alliance

Uamuzi unaondoa kizuizi kikubwa cha kufanyika majadaliano ya kumaliza vita vyilivyozuka karibu miaka miwili iliyopita.

Katika taarifa yake iliyotolewa jana Jumapili, mamlaka za jimbo la Tigray zimearifu kwamba zinajitayarisha kushiriki mchakato wa amani chini ya Umoja wa Afrika na makubaliano ya pamoja ya kusitisha mapigano jimboni humo.

Tangazo hilo limetolewa katika wakati juhudi za kidiplomasia za kimataifa zimegonga kisiki baada ya mwezi uliopita  kuzuka tena mapigano kwenye jimbo hilo la kaskazini mwa Ethiopia hali iliyotatiza mipango ya kusambazwa msaada wa kiutu.

Katika taarifa yake mamlaka za jimbo hilo zimeelezea utayari wake wa kuweka chini silaha na kutekeleza makubaliano yoyote yatakayofikiwa kutuliza hali ya mambo na kutoka nafasi ya kuanza juhudi za upatanishi.

Serikali ya Ethiopia kwa upande wake ilikwishasema kuwa iko tayari kwa mazungumzo na wapiganaji hao yatakayoratibiwa na Umoja wa Afrika.

Ilisema inataka kushiriki mazungumzo hayo wakati wowote na mahala popote bila ya kuwepo masharti yoyote mezani.

Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa zakaribisha tangazo la TPLF

Mapigano yamefanya maisha kuwa magumu jimboni TigrayaPicha: Alemnew Mekonnen/DW

Mkuu wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat  amelikaribisha tangazo la nia njema kutoka upande wa Tigray akisema ni "nafasi ya pekee kuelekea kupatikana amani" na amezitolea mwito pande zinazohusika kufikia makubaliano ya haraka ya kusitisha mapigano na kuanza mazungumzo ya moja kwa moja.

Wito sawa na huo umetolewa pia na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliyezirai pande zote kutumia nafasi hiyo kukomesha mapigano moja kwa moja na kuingia kwenye mazungumzo.

Serikali kuu mjini Addis Ababa naye imepokea kwa bashasha dhamira njema iliyotangazwa na watawala huko Tigray. Waziri anayeshughulikia amani Taye Dendea amelitaja tangazo la TPLF kuwa "mwelekeo mzuri" lakini amesisitiza ni sharti kundi la wapiganaji wa TPLF lipokonywe silaha kabla ya mazungumzo ya amani kuanza.

TPLF: Watu wa Tigray wanatarajia mazungumzo ya dhati 

Haijawa wazi ni lini hasa mazungumzo yanaweza kuanza lakini inafahamika kwamba kundi la ukombozi wa watu wa Tigray TPLF linapinga dhima ya upatanishi wa mzozo huo kupewa mjumbe maalum wa Umoja wa Afrika kwenye kanda ya pembe ya Afrika Olusegun Obasanjo.

TPLF linamtuhumu rais huyo wa zamani wa Nigeria kuwa karibu na utawala wa waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed. Haijafahamika iwapo Umoja wa Afrika itaratibu uwezekano wa kutomjumuisha Obasanjo pindi muda wa mazugumzo utakapowadia.

Tangazo la TPLF halijatoa masharti yoyote ya awali kabla ya kuanza mchakato wa kusaka amani, ingawa limesema Watigrinya watarajia mchakato wa amani wa "dhati" na wenye wapatanishi wanaokubalika na kila upande na katika Jumuiya ya Kimataifa.

Iwapo mchakato wa amani unataanza itakuwa ni mwanzo mzuri wa kumaliza machafuko kwenye mkoa wa Tigray yalizuka Novemba 2020 baada ya serikali kuu ya Ethiopia kutuma jeshi lake kwenye eneo hilo kuzima kile watawala mjini Addis Abbaba walichokitaja kuwa "uasi".