1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TPLF yasema jeshi la Ethiopia limeanza operesheni Tigray

Saleh Mwanamilongo
12 Oktoba 2021

Jeshi la Ethiopia limeanzisha operesheni maalum ya ardhini dhidi ya vikosi vya waasi wa Tigray. Msemaji wa chama cha ukombozi wa watu wa Tigray TPLF amesema hayo kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.

Äthiopien Tigray Konflikt alter Panzer
Picha: REUTERS

Wakati huohuo shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa IOM limempa likizo ya dharura mkurugenzi wake nchini Ethiopia kwa madai ya kutoa mahojiano bila idhini. 

Msemaji wa TPLF Getachew Reda ameliambia shirika la habari la Reuters kwa njia ya simu kwamba jeshi sambamba na vikosi maalum kutoka mkoa wa kaskazini wa Amhara walianzisha oparesheni yao Jumatatu asubuhi.

Soma pia: Shinikizo laongezeka dhidi ya serikali ya Ethiopia kuhusu jimbo la Tigray

Baadae taarifa ya wapiganaji wa TPLF ilisema mashambulio hayo ni pamoja ya angani, ndege zisizo na rubani na milipuko ya mabomu na silaha nzito. Hakukuwa na duru za kujitegemea kuthibitisha taarifa hizo.

Katika taarifa kwa shirika la habari la  Associated Press, msemaji wa Waziri Mkuu Abiy Ahmed, Billene Seyoum, alisema tu kwamba serikali ya Ethiopia itaendelea kukabiliana na vikosi vya Tigray ilikuzuia uharibifu, vurugu na mauaji katika mkoa wa Amhara na mahali pengine.

Mnamo mwezi Julai, wapiganaji wa TPLF walidhibiti jimbo hilo na kudai kuwakamata baadhi ya wanajeshi wa Ethiopia.Picha: Stringer/REUTERS

Soma: UN yaonya mzozo wa Tigray kuwa mbaya zaidi

Shambulio hilo jipya limekomesha mpango wa usitishaji mapigano wa upande mmoja ambao serikali ya Ethiopia iliutangaza mnamo mwezi Juni hukoTigray, ambako vikosi vyake vilikuwa vikiwasaka viongozi wa jimbo hilo, ambao walikuwa wamedhiti serikali ya kitaifa kwa miaka 27 kabla ya Abiy kuchukuwa madaraka na kuwatenga kwenye serekili yake. Maelfu ya watu wameuawa tangu mzozo wa kisiasa kugeuka kuwa vita mnamo Novemba mwaka jana.

Mapigano mapya pia yanapuuza mito ya amani iliotolewa na Umoja wa Mataifa na nchi nyingine, na kitisho cha vikwazo vipya kutoka Marekani na Umoja wa Ulaya. Taarifa ya wapiganaji wa TPLF ilisema vikosi vyao havina njia nyingine bali kuwatetea watu wao.

Wakati hayo yakijiri, Shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM, limempa likizo ya dharura mkurugenzi wake nchini Ethiopia, kutokana na kile lilichosema ni "kufanya mahojiano bila idhini", ambamo ndani yake alilalamika kutengwa na wakuu wake wanaowapendelea waasi wa jimbo la Tigray.

Umoja wa Mataifa umemuita mkuu wake wa uhamiaji wa Ethiopia Maureen Achieng (kushoto kwenye picha)Picha: DW/S. Muchie

Kuondoka kwa Maureen Achieng kulikothibitishwa na shirika la habari la AFP kunazidi kuhujumu juhudi za misaada katika wakati ambapo tayari Ethiopia imeshawafukuza maafisa wengine saba wa Umoja wa Mataifa kwa madai ya kuingilia mambo yake ya ndani.

Wiki iliyopita, rikodi za mahojiano kati ya Achieng na afisa mwengine wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa wakiwa na mwandishi wa habari, Jeff Pearce, yalisambaa mitandaoni, ambapo Achieng anawakosoa wenzake waliokimbilia Addis Ababa baada ya vita kuanza mwezi Novemba mwaka jana, na kuwatenga maafisa waliokuwepo Tigray.

Siku ya Jumatatu Antonio Vitorino, mkurugenzi mkuu wa shirika la IOM, aliandika barua kwamba maoni ya Achieng hayalihusishi shirika hilo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW