Traore aridhia mazungumzo na MNLA
31 Januari 2013Dioncounda Traore ametangaza kuwa tayari kufanya mazungumzo na kundi la waasi wa kituareg la MNLA kwa sharti kwamba kundi hilo linaachana na madai ya uhuru wa jimbo la Kaskazini.Tangazo hilo alilolitowa kupitia redio ya Ufaransa RFI limekuja wakati ambapo wiki hii kundi hilo lilisema kwamba limeudhibiti mji wa Kidal ambao ni ngome ya mwisho ya wanamgambo wa kiislamu baada ya wanamgambo hao kuukimbia.
Siku ya Jumanne wanajeshi wa Ufaransa wakaudhibiti uwanja wa ndege wa mji huo.Aidha kauli hiyo ya Traore inafuatia wito uliotolewa na Ufaransa wa kufanyika mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Bamako na wawakilishi halali wa jimbo la Kaskazini ambao ni waasi hao wakituareg wa kundi la MNLA wanaopigania ukombozi wa kile wanachokiita taifa la Azawad.Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa,Phillippe Lalliot amesema njia pekee ya itakayojenga msingi wa serikali ya Mali kurudisha utawala wake katika jimbo hilo la Kaskazini ni kupitia mazungumzo kati ya Kusini na Kaskazini,mazungumzo ambayo bila shaka yatawatenga wale wanaoitwa magaidi.
Na kwahivyo sasa rais Traore anaonekana kuutikia mwito huo na kuridhia mazungumzo hayo ambayo hayatowashirikisha wanamgambo kutoka makundi matatu ya itikadi kali za kiislamu Ansar Dine,Mujwa na Aqim ambalo ni tawi la alqeada katika eneo la Afrika ya Kaskazini.
MIA watafuta pa kukimbilia
Jumatano tarehe 30 Januari kundi lililojitenga na Ansar Dine na kujiita vuguvugu la ukombozi kwa ajili ya Azawad MIA lilidai kuudhibiti mji wa Kidal huku msemaji wake akiarifu kwamba viongozi wa kundi hilo wako katika mazungumzo na jeshi la Ufaransa katika eneo hilo.
Itakumbukwa kwamba kundi la MIA lilitangaza kujitenga kutoka kundi la Ansar Dine siku ya Jumatatu na kusema kwamba linapinga itikadi kali pamoja na ugaidi na kwamba linataka kutafuta suluhisho la mgogoro wa nchi hiyo kwa njia ya amani.Jana likatoa taarifa ya kuiomba jumuiya ya Kimataifa kuzuia hatua ya kupelekwa wanajeshi wa Mali na vikosi vya wanajeshi wa nchi za Afrika Magharibi katika jimbo la Kidal kabla ya kupatikana suluhisho la kisiasa katika mgogoro huo.
Hata hivyo rais Traore akijibu juu ya wito huo wa kundi la MIA amesema kauli yao haiwezi kuzuia chochote kwasababu kinachoonekana ni kana kwamba kundi hilo linatafuta njia ya kutorokea baada ya kuona maji yamezidi unga,akasisitiza kwamba kundi pekee linalozingatiwa kuingia kwenye mazungumzo ya kusaka amani ni MNLA na ikiwa tu kundi hilo litasalimu amri ya kudai uhuru wa Kaskazini.
Wakati huohuo Ufaransa imetangaza kuunga mkono pendekezo la kutumwa kikosi cha kuweka amani cha Umoja wa Mataifa nchini Mali huku waziri wa ulinzi wa nchi hiyo Jean-Yves Le Drian akisema nchi yake itabeba jukumu katika mpango huo.Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kujadiliana uwezekano wa kuchukua hatua hiyo.
Mwandishi Saumu Mwasimba
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman