Trapp arejea Eintracht Frankfurt
31 Agosti 2018"Nina shauku kubwa ya kuuona mwaka mwingine nikiwa na Frankfurt," alisema mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 28 ambaye aliichezea Eintracht Frankfurt kuanzia mwaka 2012 hadi 2015 kabla ya kujiunga na PSG kwa kitita cha euro milioni 10.
Frankfurt ilimpata Trapp masaa kadhaa kabla ya dirisha la usajili kufungwa nchini Ujerumani na Ufaransa na atacheza katika pambano la Jumamosi la Bundesliga dhidi ya Werder Bremen.
Trapp, mlinda mlango wa tatu wa timu ya taifa ya Ujerumani nyuma ya Manuel Neuer na Marc-Andre ter Stegen , pia alijikuta akiwa namba tatu katika kikosi cha PSG nyuma ya Gianluigi Buffon na Alphonse Areola msimu huu. Alirukia fursa ya kujiunga na Frankfurt kwa msimu wa 2018 / 19. "Wakati nilipokuwa Paris, nilikuwa nakumbuka sana wakati mzuri nilipokuwa Frankfurt," alisema Trapp, ambaye amecheza mara tatu katika lango la timu ya taifa ya Ujerumani tangu Juni 2017.
"Mahusiano hayakuvunjika na nilifurahi sana wakati Eintracht iliposhinda kombe la Ujerumani, DFB Pokal," aliongeza, akimaanisha ushindi wa kushitua wa frankfurt wa mabao 3-1 dhidi ya Bayern Munich katika fainali mwezi Mei mwaka huu.
"Ni muhimu kwangu mimi kuwapo katika mazingira ambako najisikia vizuri na ambako naweza kucheza."
Trapp , ambaye alikuwa sehemu ya timu ya taifa ya Ujerumani katika kombe la dunia ambayo iliondolewa na mapema katika awamu ya makundi, anaweza kuingia moja kwa moja katika kikosi cha kwanza cha Frankfurt kwa kuwa mlinda mlango wao namba moja raia wa Denmark Frederik Ronnow akiwa majeruhi baada ya kuumia goti.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Iddi Ssessanga