Trump aachana na sera ya kuzitenganisha familia za wahamiaji
21 Juni 2018Trump ametia saini agizo linaloziruhusu familia za wahamiaji zizuiwe pamoja zinapokamatwa zikiingia Marekani kinyume na sheria hadi kesi zao zitakapoamuliwa.
Kiongozi huyo wa Marekani amesema lengo ni kuhakikisha familia hazitenganishwi lakini wakati huo huo, wanahakikisha mipaka inalindwa kwa mfumo madhubuti kuzuia mmiminiko wa wahamiaji nchini Marekani na kuwa alisikiza ushauri kutoka kwa mke wake Melania na binti yake Ivanka kufikia uamuzi huo wa kulegeza kamba.
Trump alegeza kamba
Trump amesema amesikiliza kwa makini ushauri wa binti yake Ivanka ambaye pia ni mshauri wake kuhusu sera hiyo na kuongeza kuwa imezua hisia kutoka kwa kila aliye na imani na huruma akiwemo yeye.
Afisa mmoja wa Ikulu ya White House mjini Washington, amesema mke wa kiongozi huyo wa Marekani Melania, katika mazungumzo ya faragha na mume wake alimuomba achukue hatua kukomesha mzozo huo wa kibinadamu.
Mapema wiki hii, Melania pamoja na wake wa marais wa zamani wa Marekani walitoa wito wa kusitishwa kwa sheria hiyo ya kuwatenganisha wazazi wahamiaji na watoto wao wakisema Marekani inapaswa kuongozwa kwa kuzingatia sheria lakini pia kwa kuwa na imani.
Licha ya kuwa agizo hilo linafikisha kikomo sera ya kuzitenganisha familia iliyolaaniwa vikali na viongozi mbali mbalii akiwemo Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis na mashirika ya kutetea haki za binadamu, inamaanisha kuwa watoto watasalia vizuizini kwa muda usiojulikana.
Utawala wa Trump unakabiliwa na changamoto za kisheria kwa sababu uamuzi wa mahakama unawianisha kuwa maafisa wa uhamiaji wanaweza tu kuwazuia watoto kwa muda usiozidi siku ishirini na hilo huenda likachochea upya upinzani dhidi ya sera kali za Trump kuhusu uhamiaji, sera ambazo aliahidi kuzitekeleza wakati wa kampeini za uchaguzi wa rais mwaka.
Sera za kutenganisha familia zatajwa katili
Maafisa wa serikali bado hawajafafanua iwapo kutenganishwa kwa familia kutakoma mara moja au lini na vipi familia zilizotenganishwa zitakutanishwa tena na jamaa zao.
Video zilizovujishwa wiki hii zilionesha watoto wakilia wakiwa vizuizini na kupelekea utawala wa Trump kulaaniwa vikali na Wamarekani na jumuiya ya kimataifa. Inakadiriwa zaidi ya watoto 2,000 walitenganishwa na wazazi wao katika kipindi cha wiki sita zilizopita kati ya tarehe 5 Mei na tarehe 9 mwezi huu.
Serikali za nchi za Amerika ya kati na Mexico zimepokea vyema uamuzi wa Trump wa kubatilisha sera yake ya kuzitenganisha familia lakini zimesema zitasalia kuwa macho ili kuhakikisha haki za raia wao zinaheshimiwa.
Duru kutoka Ikulu ya rais imesema Trump anatambua kuwa suala la kuzitenganisha familia ni tatizo la kisiasa linalokua. Hatua ya Trump ya kubatilisha uamuzi aliokuwa amechukua kuhusu uhamiaji ndiyo mara ya kwanza kwake kubadilisha msimamo tangu aingie madarakani Januari 2017.
Mwandishi: Caro Robi/Reuters
Mhariri: Daniel Gakuba