1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump aahidi kuwazuia wahamiaji kuingia Marekani

20 Januari 2025

Donald Trump ameahidi kuchukua hatua kadhaa za kuzuia kile alichokiita "kuanguka kwa Marekani" mara tu atakapoapishwa rasmi kama rais wa nchi hiyo Jumatatu.

USA I Washington - Donald Trump
Rais mteule Donald TrumpPicha: Matt Rourke/AP/picture alliance

Akiwahutubia wafuasi wake walioujaza uwanja wa michezo wa One Sports Arena huko Washington usiku wa kuamkia Jumatatu katika mkutano wa kusherehekea ushindi wake, Trump amesema atakabiliana na wahamiaji.

"Tutasitisha kuvamiwa kwa mipaka yetu," alisema Trump.

Trump hususan amewataja wahalifu kama sehemu ya wimbijipya la wahamiaji kutoka Venezuela. Ameahidi kuwaondoa nchini Marekani wanachama wa genge la Venezuela la Tren de Aragua.

Wafuasi wa Trump mjini Washington Picha: Celal Gunes/Anadolu/picture alliance

"Hawa ni watu wabaya na wataondoka nchini mwetu," rais huyo mteule alisema.

Sehemu kubwa ya hotuba ya saa moja nzima ya Trump imejikita katika uhamiaji, akisisitiza hoja ambayo ilimpelekea kupata ushindi mkubwa dhidi ya mpinzani wake Kamala Harris katika uchguzi wa mwezi Novemba.

Ni ipi mipango ya Trump ya siku ya kwanza?

Trump ameahidi kusuluhisha "kila tatizo" linaloikabili Marekani na kuweka amri kadhaa mpya katika siku zake za kwanza za urais wake.

"Katika historia ya Marekani, tutakuwa na siku bora zaidi ya kwanza ya urais, wiki bora zaidi ya kwanza na siku bora zaidi 100 za kwanza kuwahi kushuhudiwa," alisema Trump.

Rais huyo mteule alisema atazitoa "rekodi zilizosalia kuhusiana na mauaji" ya Rais wa zamani wa Marekani John F. Kennedy, Seneta Robert Kennedy na mwanaharakati wa haki za kiraia Martin Luther King Jr.

Kabla kuingia madarakani mwaka 2017, Trump alitoa ahadi sawa na hizo ila akaishia kutoa nyaraka kadhaa tu za siri zinazohusiana na mauaji hayo.

Walinda usalama nje ya majengo ya bunge Marekani kuelekea kuapishwa kwa TrumpPicha: Ting Shen/Xinhua/picture alliance

Trump vile vile ameahidi kuchukua hatua kuhakikisha kwamba wanaume hawajihusishi na michezo ya wanawake mara baada ya kuchukua hatamu za uongozi Jumatatu.

Trump anatarajiwa kuapishwa rasmi kama rais wa 47 wa Marekani mwendo wa saa sita mchana kwa saa za mjini Washington.

Trump mwenye umri wa miaka 78, alikuwa jukwaani na bilionea Elon Musk ambaye ataongoza juhudi za kupunguza matumizi katika serikali yake.

Musk aliapa kuifanya Marekani kuwa nchi yenye nguvu kwa karne nyingi zijazo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW