Trump aapa kupambana mahakamani
1 Aprili 2023Muda mchache baada ya mahakama kuamua kuwa Trump, mwenye umri wa miaka 76, ana kesi ya kujibu, na anayekusudia kuwania tena urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2024 aliwashambulia waendesha mashitaka walioyaibua mashitaka haya dhidi yake na hata jaji anayetegemewa kusikiliza kesi yake.
Akitumia mtandao wake wa kijamii, Truth Social, Trump aliandika kwa herufi kubwa: "UINGILIAJI WA UCHAGUZI, MAHAKAMA YA KANGAROO!" Aliongeza pia Jaji Manuel Marchal atakayesimamia kesi yake "ananichukia."
Soma zaidi: Trump kushtakiwa kufuatia malipo kwa Stormy Daniels
Jioni ya siku ya Jumanne (Aprili 4), Trump anatazamiwa kufunguliwa rasmi mashitaka, kuchukuliwa alama za vidole na kupigwa picha na bango la mashitaka kwenye mahahakama ya Manhattan kabla ya kupandishwa kizimbani akiwa rais wa kwanza wa Marekani kukabiliana na mashitaka ya uhalifu.
Kutiwa pingu
"Rais Trump hatatiwa pingu," alisema Joe Tacopina, mmoja wa mawakili wa Trump, akiongeza kwamba haamini kwamba waendesha mashitaka "wataruhusu suala hili kuwa maonesho."
Tacopina alisema kesi ya fedha za fidia iliyoletwa na Mwendesha Mashitaka wa Wilaya ya Manhattan, Alvin Bragg, dhidi ya Trump ina mapungufu mengi kisheria na rais huyo wa zamani angelikana kutenda uhalifu wowote.
Soma zaidi: Usalama waimarishwa mjini New York
"Hakuna uwezekano wowote kwa Trump kukubali kusaka suluhisho kwa kukiri kosa. Hilo halitatokea. Hapana uhalifu uliotendeka hapa." Alikiambia kituo cha televisheni cha NBC.
"Trump, ambaye kwa sasa yupo kwenye makaazi yake ya Mar-a-Lago mjini Florida, awali alishitushwa na uamuzi wa mahakama hiyo, lakini kwa sasa amerudi kwenye hali ya kawaida na yuko tayari kupambana." Alisema wakili huyo.
Safari ya White House mashakani
Uwezekano wa Trump kuwekwa kizuizini kunaongeza mashaka kwenye kampeni yake ya kuwania kurejea kwenye Ikulu ya White House.
Hasimu wake, Rais Joe Biden, amekwepa kuzungumza chochote kuhusiana na kesi hiyo.
Jopo la majaji jijini New York lilimuona Trump ana kesi ya kujibu siku ya Alhamis (Machi 30) kwa malipo ya fedha taslimu dola 130,000 aliyoyafanya kwa mchezaji wa filamu za ngono ili kumnyamazisha wakati wa kampeni zake za urais mwaka 2016.
Soma zaidi: Biden akataa kuzungumzia mashitaka dhidi ya mtangulizi wake Trump
Trump amekana kutenda kosa lolote na amemtuhumu Bragg, mwanachama wa chama cha Democrat, kwa kuendeleza vita vya kisiasa ili kumzuwia kwenye kampeni yake ya kurudi madarakani.
Awali Trump aliitisha maandamano ya wafuasi wake akionya kwamba kesi dhidi yake inaweza kupelekea "kifo na maangamizo ya nchi."
Kwenye taarifa yake, rais huyo wa zamani alisema alishakusanya dola milioni 4 kwa ajili ya kampeni yake ya uchaguzi ndani ya kipindi cha masaa 24 baada ya habari ya kesi yake kutangazwa.