1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump adai kirusi cha corona kilianzia maabara ya China

Josephat Charo
1 Mei 2020

Rais wa Marekani Donald Trump amesema ameona ushahidi kwamba kirusi kipya cha corona kilianzia katika maabara ya China.

USA Coronavirus Donald Trump
Picha: Reuters/C. Barria

Kauli ya Trump ilipunguzwa makali na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo aliyesema, "Hatujui hasa kirusi cha corona kilipoanzia." Hata hivyo mada ya Trump, ambayo tayari yamekanushwa na China, yumkini yakachochea wasiwasi wakati shirika la afya dunaini WHO likiomba liruhusiwe kushiriki katika uchunguzi unaofanywa na China kuhusu walikotokea wanyama waliosababisha mlipuko wa aina mpya ya kirusi cha corona.

Msemaji wa WHO, Tarik Jasarevic, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba shirika hilo linaelewa kuna uchunguzi unazoendelea China kuelewa vizuri zaidi chanzo cha mlipuko huo, lakini akaongeza WHO kwa sasa haishiriki katika tafiti hizo za China.

Jasarevic amekiambia kikao cha Umoja wa Mataifa mjini Geneva  leo kwamba mkutano wa kila mwaka wa shirika la WHO unaowaleta pamoja mawaziri wa afya utafanyika Mei 18 kwa njia ya video, mada kuu katika ajenda ikituwama juu ya gonjwa la COVID-19.  Ajenda fupi ya mkutano huo itajumuisha masuala ya kuendeleza utawala kama uchaguzi wa wanachama wa kamati ya utendanji na hotuba ya mkurugenzi wa WHO Tedros Adhanom Ghebreysus.

Kwa upande mwingine shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia watoto la UNICEF limetoa mwito lisaidiwe kusambaza shehena za chanjo kufuatia kupungua kwa kiwango kikubwa safari za ndege na uhaba wa ndege ndogo binafasu wakati huu wa zilzala la corona.

Msemaji wa UNICEF, Marixie Mercado amezitaka serikali, sekta binafsi, sekta ya usafiri wa anga na nyinginezo, kuruhusu usafirishaji wa mizigo kwa gharama nafuu kwa chanjo zinazonuiwa kuyaokoa maisha ya watu.

Guterres aikosoa jumuiya ya kimataifa kwa kutoisadia Afrika

Wakati haya yakiarifiwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekosoa mapungufu yaliyojitokeza katika uratibu na ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na athari za virusi vya corona barani Afrika.

"Nina wasiwasi mkubwa hasa kwa eneo la kusini la dunia, yaani bara la Afrika. Katika nchi za Afrika janga la corona lilifika kuchelewa. Nina wasiwasi pia kuhusu nchi ambazo zinakabiliwa na kitisho kikubwa kutokana na mifumo yao dunia ya kijamii na kiuchumi. Hakukuwa na hatua za kutosha za mshikamano kutoka kwa jumuiya ya kimataifa kuzisaidia nchi hizi, ili ziweze kujenga haraka uwezo wa kupambana na janga la corona na kuzilinda chumi zao dhidi ya athari mbaya za ugonjwa wa covid 19"

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa MataifaPicha: webtv.un.org

Guterres aidha amesema ana wasiwasi kuhusu hali itakavyoendelea katika mataifa ya Afrika akihofia huenda janga hili likaenea mithili ya moto wa mwituni likisababisha athari kubwa zitakazoyavuruga maisha ya watu na hususan chumi dhaifu. Ameonya kwamba kuna kitisho janga hili katika siku za usoni likalipuka tena eneo la kaskazini la dunia baada ya kusababisha zilzala katika mataifa ya kusini.

Alisema leo kunashuhudiwa mahusiano ya kimaitafa yakidumazwa na malumbano na mashindano kati ya dola kubwa duniani huku changamoto zikishuhudiwa katika kundi la nchi zilizostawi kiviwanda duniani G7 na kundi la nchi zilizostawi kiuchumi na zinazoinukia kwa kasi kiuchumi la G20.

Comoro yathibitisha kisa cha kwanza cha corona

Kauli ya Guterres ilikuja wakati Comoro ikithibitisha kisa cha kwanza cha maambukizi ya virusi vya corona. Rais wa Comoro Azali Assoumani amesema wakati wa hotuba kwa taifa kwamba aliyeambukizwa ni mwanamume mwenye umri wa zaidi ya miaka 50 aliyekuwa na maingilia ya karibu n raia wa Ufaransa mwenye asili ya Comoro ambaye alisafiri hivi karibuni nchini Ufaransa. Azali amesema hali ya mgonjwa huyo inaimarika pole pole na kuongeza kuwa watu wote waliokutana naye wanafuatiliwa.

Visiwa vya Comoro na Ufalme wa Lesotho ndizo nchi mbili pekee barani Afrika ambazo hazikuwa na maambukizi ya virusi vya corona. Sasa imebaki Lesotho pekee.

Hatua kali za kufunga shughuli za kila siku na kuwazuia watu kubakia majumbani mwao zimeendelea kulegezwa leo, huku Afrika Kusini na Austria zikiruhusu baadhi ya biashara kufunguliwa tena, na hivyo kujiunga na sehemu nyingine za Ulaya na baadhi ya majimbo ya Marekani ambayo yameanza kuruhusu maisha ya kawaida katika siku chache zilizopita.

dpae, afpe, rtre

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW