1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump ateuwa wafuasi wenye msimamo mkali nyadhifa kuu

12 Novemba 2024

Rais mteule wa Marekani, Donald Trump, ametangaza wajumbe wapya wa serikali ijayo, na anatarajiwa kumchagua Seneta Marco Rubio kuwa waziri wa mambo ya nje, na Michael Waltz, kuwa Mshauri Mkuu wa Usalama wa Taifa.

Donald Trump
Rais Mteule wa Marekani Donald Trump ameanza kusuka safu yake ya viongozi kwa kuwateua baadhi ya wafuasi wake kinda kinda na wenye msimamo mkali.Picha: Callaghan O'Hare/REUTERS

Wateule hao wawili kutoka Florida watakuwa watu muhimu katika utekelezaji wa sera ya mambo ya nje ya Trump ya "Amerika Kwanza," ambapo rais huyo mteule ameahidi kumaliza vita vinavyoendelea nchini Ukraine na Mashariki ya Kati na kuepuka kuihusisha zaidi Marekani katika mizozo ya kijeshi.

Trump, tajiri wa miaka 78 kutoka chama cha Republican, ameahidi kipindi chake cha pili madarakani kitaleta mabadiliko makubwa katika serikali ya shirikisho.

Trump pia alimtangaza Tom Homan kuwa mdhibiti mkuu wa mipaka, akimpa jukumu la kutimiza ahadi yake kuu ya sera ya ndani ya kufukuza wahamiaji wengi wasio na vibali.

Mbunge Elise Stefanik kutoka New York, mtetezi wa Israel, aliteuliwa kuwa balozi wa Umoja wa Mataifa, huku Lee Zeldin akiteuliwa kuwa mkuu wa Shirika la Kulinda Mazingira, EPA, ili kupunguza kanuni za hali ya hewa na uchafuzi ambazo zinaonekana kuwa vikwazo kwa biashara.

Trump akiwa na Marco Rubio ambaye anatazamiwa kumteua katika wadhifa wa Waziri wa Mambo ya Nje.Picha: Evan Vucci/AP Photo/picture alliance

Wateuliwe wa juu, wakiwemo Elise Stefanik, Lee Zeldin, na Marco Rubio kama waziri wa mambo ya nje, watahitaji kuidhinishwa na Seneti. Hata hivyo, Trump anatumaini kukwepa uangalizi wa Seneti kwa kufanya uteuzi wakati Seneti ikiwa katika mapumziko.

Soma pia: Rais mteule wa Marekani Donald Trump amemteua Mike Waltz kuwa mshauri wa Usalama wa Taifa

Amegeuza suala hili kuwa mtihani wa utiifu, akisisitiza siku ya Jumamosi kuwa mrepbulican yeyote anaetaka kuwa kiongozi wa Seneti lazima akubaliane na uteuzi wa kipindi cha mapumziko.

Trump aendeleza ajenda ya utiifu

Trump anajulikana kwa kudai utiifu kamili kutoka kwa wasaidizi na wateule wake serikalini, ambapo wote aliowateuwa wakiwa wale waliomtetea na kuunga mkono madai yake yasiyo na msingi kuhusu udanganyifu wa uchaguzi baada ya kushindwa na Rais Joe Biden mwaka 2020.

Uteuzi wa Marco Rubio utahitimisha mabadiliko ya ajabu katika uhusiano kati ya watu hao wawili, ambao hapo awali walikuwa na uhasama wakati wa kugombea uteuzi wa urais wa chama cha Republican mwaka 2016.

Rubio, ambaye ana asili ya Cuba, alianza kujulikana katika sera za kigeni kama mpinzani mkali wa serikali ya Cuba na washirika wake wa mrengo wa kushoto huko Amerika ya Kusini, hususan Venezuela.

Kwa sasa, Rubio ni mmoja wa maseneta wanaoikosoa vikali China, akijaribu kuzuia kampuni za China kufanya biashara nchini Marekani na kuongoza juhudi za bunge kuadhibu China kuhusu haki za binadamu, hususan kwa na namna inavyowatendea jamii ya wachache wa kabila la Uyghur.

Howad Lutnick ameteuliwa kusimamia uhamiaji na mipaka ya Marekani, akiwa na jukumu la kuwatimua makumi kwa maelfu ya wahamiaji wasio na vibali halali vya kuishi Marekani.Picha: Evan Vucci/AP Photo/picture alliance

Tom Homan, anayetarajiwa kuwa mkuu wa masuala ya uhamiaji na mipaka, aliwahi kuwa mkurugenzi wa muda wa Idara ya Uhamiaji na Forodha, ICE, chini ya Trump.

Soma pia: Je, ni kwa kiasi gani Warepublican wanaweza kubadilisha Marekani?

Trump alisema Homan ndiye bora zaidi katika kudhibiti mipaka ya Marekani na atakuwa na jukumu la kuratibu operesheni kubwa ya kufukuza wahamiaji wasio na vibali katika historia ya Marekani.

Homan ni mtetezi wa muda mrefu wa ajenda ya Trump ya kurejesha ukuu wa taifa la Marekani - maarufu kama "Make America Great Again."

Trump amemteua Susie Wiles kuwa mkuu wa wafanyakazi wa Ikulu ya White House, nafasi isiyohitaji kuthibitishwa na Seneti.

Warepublican wanatarajiwa kuwa na wingi mkubwa katika Seneti na huenda wakapata wingi katika Baraza la Wawakilishi, jambo ambalo litampa Trump uhuru wa kutekeleza ajenda yake.

Trump amemteua Lee Zeldin kuwa mkuu wa idara ya mazingira, akimpa jukumu la kufanya maamuzi ya haraka ya kufuta kanuni ambazo Trump anaamini zinazuia biashara.

Chanzo: AFPE