1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump afunguwa mashitaka kupinga kuitwa mbele ya Congress

12 Novemba 2022

Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, anaishitaki kamati ya bunge inayochunguza mashambulizi ya Januari 6 dhidi ya jengo la bunge akijaribu kuzuwia kuitwa kwenye kamati hiyo kutoa ushahidi wake.

USA I Midterm 2022 I Donald Trump in Palm Beach
Picha: Joe Raedle/AFP/Getty Images

Hati ya mashitaka iliyoonekana na shirika la habari la AP inahoji kwamba ingawa marais wengine wa zamani wamewahi kujitolea kwa hiari yao kutowa ushahidi ama nyaraka kwa maombi ya bunge, lakini "hakuna rais aliyepo madarakani ama wa zamani aliyewahi kulazimishwa kufanya hivyo."

"Kigezo cha muda mrefu na uhalisia unaonesha kwamba mgawanyo wa madaraka unalizuwia bunge kumlazimisha rais kutowa ushahidi mbele yake," alisema wakili wa Trump, David A. Warrington, kwenye taarifa ya kutangaza dhamira ya mteja wake.

Alisema Trump ameshirikiana na kamati ya bunge kwa nia njema katika jitihada za kumaliza wasiwasi uliopo baina ya tawi la utawala na mtengano wa madaraka," lakini alisema jopo hilo "linasisitiza kutumia njia ya kisiasa, na hivyo kumfanya Trump asiwe na njia nyengine isipokuwa kuelekea kwenye mkono wa tatu, yaani mahakama, kwenye mzozo huu baina ya mkono wa utawala na wa bunge."

Mashitaka hayo yanaweka kiwingu kwenye uwezekano wa Trump kulazimika kutoa ushahidi kutokana na ukweli kwamba kamati yenyewe imepangiwa kuvunjwa mwishoni mwa kipindi cha bunge kinachokamilika mwezi Januari. 

Kamati hiyo ilipiga kura kwa kauli moja kutaka Trump apewe hati ya kuitwa bungeni wakati wa kikao chake cha mwisho kilichotangazwa moja kwa moja kwa njia ya televisheni kabla ya chaguzi za katikati ya muhula, na mwezi uliopita ikaandika rasmi barua ya kutaka ushahidi wa rais huyo wa zamani.

Tuhuma dhidi ya Trump

Picha inayomuonesha Rais Joe Biden (kushoto) na mpinzani wake Donald Trump.

Wajumbe wa kamati hiyo wanadai kuwa mwenyewe Trump alishiriki kwenye matukio kadhaa ya kubadilisha matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2020. 

Wanamtaka ama atowe ushahidi wake mbele ya kamati katika jengo la Capitol yaliko makao makuu ya Congress au kwa njia ya video "kuanzia tarehe 14 Novemba" na kuendelea kwa siku kadhaa kama itakavyohitajika.

Barua hiyo pia iliorodhesha maombi mengine ya nyaraka, yakiwemo mawasiliano binafsi kati ya Trump na wajumbe wa baraza la Congress na pia makundi ya siasa kali.

Kwenye mashitaka yake, mawakili wake wanaikosowa hati ya kumuita Trump kutoa ushahidi kama ya jumla jamala na wanaitaja kama uingiliaji kati wa haki zake za kikatiba.

Pia wanahoji kwamba vyanzo vyengine, kando ya Trump, vinaweza kutoa taarifa hizo hizo zinazotakiwa na kamati ya bunge na hivyo hakuna ulazima wa mteja wao kuhudhuria mbele ya kamati ya bunge.

Mashitaka hayo yanakuja wakati Trump akitazamiwa kuzinduwa kampeni ya tatu kuwania urais wiki ijayo.

Yalifunguliwa kwenye Wilaya ya Kusini ya Florida, ambako wanasheria wake wengine walifanikiwa kufunguwa mashitaka ya kumpata mtu aliyepewa jukumu ya kupitia nyaraka zilizochukuliwa na shirika la ujasusi wa ndani la FBI kutoka nyumba ya Trump ya Mar-a-Lago mnamo tarehe 8 Agosti.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW