Trump afuta misaada kwa wanaotoa mimba
2 Februari 2017Hatua ya Rais Trump itayaathiri mashirika ya Kimarekani yanayotoa misaada nchi za nje. Lakini upinzani wake dhidi ya utoaji mimba litakuwa ni jambo gumu kulifuatilia kisheria katika nchi nyingi zinazoendelea, kwa sababu sheria ziliopo,unyanyapaa na umasikini. Mwanaharakati Rosemarry Olale kutoka Kenya ambaye husaidia kuwafunza wasichana katika maeneo ya wakaazi masikini mno mjini Nairobi, juu ya elimu ya uzazi,anasema wanawake watalazimika kutafuta njia nyengine kutoa mimba ambazo hazitakua za usalama.
Taifa hilo la Afrika mashariki ni miongoni mwa zile zenye kiwango cha juu cha utoaji mimba duniani na nyingi huwa si salama, zikisababisha majeraha na mauti miongoni mwa wanawake. Kwa mujibu wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa, kuna wanawake 21.6 milioni duniani kote ambao hutoa mimba kwa njia zisizo salama kila mwaka na 9 kati ya 10 hufanyika katika nchi zinazoendelea.
Utoaji mimba hatari kuongezeka
Mashirika yanayosaidia wanawake kutoa mimba na kuhakikisha wako salama, ni pamoja na Shirikisho la kimataifa libnalojulikana kama Planned Parenthood Federation na Marie Stopes, ambayo ni miongoni mwa yatakayoathirika kutokana na uamuzi wa Trump kupiga marufuku ufadhili wa mashirika yanayosaidia wanawake katika hilo. Maafisa wa mashirika hayo mawili wanasema bila ya ufadhili , kutakuweko na utoaji mimba milioni 2.1 katika njia zisizo salama na vifo 71,700 kutokana na uzazi, katika kipindi cha kwanza cha utawala wa Trump, jambo ambalo kimsingi linaweza kuzuiwa na kuepusha athari na maisha ya wanawake.
Shirika la Marie Stopes limekuwa likipokea dola milioni 30 kila mwaka kutoka Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kwa ajili ya kuwasaidia wanawake juu ya huduma za mipango ya familia. milioni moja na nusu katika zaidi ya nchi 12. Sasa huduma hizo zitabidi zipunguzwe, ikiwa fedha hazitopatikana.
Sheria inayojirudia
Wanawake wanaoishi katika maeneo ya vijijini bila ya huduma za serikali wataathirika zaidi. Afisa Maaike van Min kutoka Shirika hilo la Marie Stopes anazitaja miongoni mwazo kuwa ni Nigeria na Madagascar ambako Shirika hilo lina miradi mikubwa .
Mkurugenzi wa Afrika wa kituo kinachotetea haki ya uzazi Evelyne Opondo anakumbusha juu ya huduma nyingi zilizoathrika nchini Kenya baada ya Rais George W. Bush kuingia madarakani 2001 na kuirejesha sheria ya kupiga marufuku kufadhili utoaji mimba. Na sasa chini ya Trump hatua hiyo ilioodolewa baada ya Bush kuondoka madarakani , sasa inarudi tena. Mashirika husika yakalazimika pia kupunguza huduma kwa wahanga wa matumizi ya nguvu kingono na wenye virusi vya Ukimwi (HIV).
Utafiti wa Shirika la Afya Duniani pamoja na hayo, unasema kiwango cha utoaji mimba katika kanda ya Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara wakati wa utawala wa Bush kiliongezeka. Bibi Opondo anasema "inasikitisaha kwamba maisha na afya za wanawake zinawekwa reheani, kutokana na sera za Marekani." Anasema Huo ni ukosefu wa uadilifu na kutothamini utu wa binaadamu."
Mwandishi: Saumu Mwasimba (Thomson Reuters Foundation )
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman