Trump ahimizwa kulinda mazingira
17 Novemba 2016Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry ametilia mkazo athari zitakazojitokeza iwapo viongozi wa dunia watajikokota katika kupunguza kiwango cha gesi chafu inayotoka viwandani huku nchi masikini nazo zikieleza jinsi zilivyo hatarini kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi. Akizungumza hapo jana katika mkutano wa kimataifa uliondaliwa na Umoja wa Mataifa kuhusu mazingira, ambao unaendelea mjini Marrakesh, Morocco, Kerry amesema ipo siku ambapo hata walio na mashaka makubwa kuhusu haja ya kuyaokoa mazingira watakiri kuwa kuna jambo la kutisha linaloendelea kutokana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.
Donald Trump kabla ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Marekani aliyataja mabadiliko ya hali ya hewa uongo mtupu unaoenezwa na China na kuapa kufutilia mbali makubaliano ya kihistoria yaliyofikiwa mwaka jana mjini Paris ya kupunguza joto duniani. Kampuni zaidi ya 360 na wawekezaji 500 kutoka Marekani wameandika waraka wa kuwataka viongozi wa kisiasa wa Marekani kuunga mkono kikamilifu makubaliano ya Paris ambayo yananuia kuhakikisha ongezeko la joto duniani halizidi nyuzi 2 za Celsius ikilinganishwa na hali ya kabla ya mapinduzi ya viwanda.
Nchi zilizostawi zaidi kiviwanda ikiwemo Marekani zimeahidi kupunguza gesi chafu kwa kuelekea katika matumizi ya nishati safi lakini Trump ameahidi kuimarisha matumizi ya mafuta, gesi na makaa viwandani. Wataalamu wa mazingira wanaonya joto la ulimwengu linaelekea kupanda kwa nyuzi joto 3 Celsius huku viwango vya maji baharini vikiongezeka, vimbunga, ukame, magonjwa na mizozo inayochochewa na kugombania raslimali adimu pia ikiongezeka duniani.
Afrika yazungumza kwa sauti moja
Viongozi wa Afrika pia walikutana jana kukubaliana kuwa na msimamo mmoja kuhusu namna ya kukabiliana na kuongezeka kwa viwango vya joto katika bara la Afrika. Mfalme wa Morocco Mohammed wa sita aliuambia mkutano wa kilele wa viongozi zaidi ya 20 wa Afrika kuwa bara hilo linaathirika vibaya kutokana na masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa na bila shaka ndilo lililoathirika zaidi kwani linarejesha nyuma maendeleo na kutishia haki za kimsingi za mamilioni ya waafrika.
Mfalme huyo wa Morocco ameitaka Afrika kuzungumza kwa kauli moja na kutaka kuwa na haki za mazingira. Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon na Rais wa Ufaransa Francois Hollande. Ban amesema Afrika iko katika mstari wa mbele katika vita dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa na kuwa kati ya nchi 50 zilizoathirika na ongezeko la joto duniani, 36 ni za Afrika. Hollande alisema mkutano huo wa Marrakesh utaweka misingi ya mipango ya kuisaidia Afrika kifedha kuanzia mwaka 2020.
Mwaka jana kuliafikiwa kutakuwa na mfuko wa dola bilioni 100 kuzisaidia nchi masikini kuweka miundombinu ya nishati endelevu kuanzia mwaka 2020. Viongozi wa Afrika wanataka nchi zao zitengewe fedha zaidi ili kuchukua hatua madhubuti za kuyaokoa mazingira.
Mwandishi: Caro Robi/afp
Mhariri: Gakuba Daniel