Trump aikosoa jumuiya ya kujihami ya NATO
28 Machi 2016Trump alisema muungano wa kijeshi wa NATO umepitwa na wakati na kupendekeza ufanyiwe mageuzi. Trump pia alisema jumuiya ya NATO yenye nchi 28 wanachama iliundwa wakati wa enzi tofauti wakati kitisho kikubwa kwa nchi za magharibi kilikuwa ni muungano wa zamani wa Sovieti. "NATO haina uwezo wa kupambana na ugaidi na inaigharimu Marekani fedha nyingi mno," akaongeza kusema mgombea huyo.
Kauli hiyo ameitoa siku chache kabla kufanyika mkutano wa kilele wa viongozi wa dunia mjini Washington kuhusu usalama wa silaha za nyuklia. Rais wa Marakani Barack Obama atauandaa mkutano huo siku ya Alhamisi na Ijumaa wiki hii utakaowaleta pamoja wajumbe 56. Huku mkutano huo ukitarajiwa kujikita katika kutafuta njia za kuepusha mashambulizi ya kigaidi dhidi ya vituo vya nykulia, mapendekezo ya Trump huenda yakajadiliwa pia, hususan pembezoni mwa mkutano. Urusi haitahudhuria mkutano wa mjini Washington, lakini rais wa China, Xi Jinping atahudhuria.
Machi 21 mwaka huu Trump alisema Marekani inatakiwa ipunguze ufadhili wake kifedha kwa NATO, iliyoundwa mwaka 1949 baada ya vita vikuu vya pili vya dunia na kuwa ukuta wa ulinzi dhidi ya utanuzi wa muungano wa Sovieti.
Mgombea hasimu wa Trump kwa uteuzi wa chama cha Republican seneta wa jimbo la Texas, Ted Cruz, aliyaeleza maoni ya Trump kuhusu NATO kuwa ya kipuuzi. Cruz alisema kuliacha bara la Ulaya, kujiondoa kutoka kwa muungano uliofanikiwa zaidi katika nyakati za sasa, hakuna maana yoyote, akiongeza kuwa kufanya hivyo kutampa ushindi mkubwa rais wa Urusi, Vladimir Putin, na kundi la Dola la Kiislamu IS.
Katika hatua nyingine inayoondokana kabisa na sera ya kihistoria ya Marekani, Trump alisema katika mahojiano yaliyochapishwa jana na gazeti la New York Times kwamba atazingatia kuiachia Japan na Korea Kusini zitengeneze silaha zao za nyuklia, badala ya kuitegemea Marekani izilinde kutokana na kitisho cha Korea Kaskazini na China.
Trump kuziruhusu Japan na Korea Kusini kwa na nyuklia
Katika mahojiano hayo Trump alisema atakuwa tayari kuwaondoa wanajeshi wa Marekani kutoka Japan na Korea Kusini mpaka nchi hizo mbili zilipe fedha zaidi kuwahudumia na kuwalisha. Marekani ina wanajeshi 50,000 nchini Japan na wengine 28,500 nchini Korea Kusini.
Waziri kiongozi wa Japan, Yoshihide Suga, ameuambia mkutano wa waandishi wa habari leo mjini Tokyo kwamba hakujafanyika mageuzi ya sera ya Japan ya kutojenga, kumiliki au kuanzisha silaha za nyuklia na akasisitiza bila kujali nani atakayekuwa rais wa Marekani, uhusiano kati ya Marekani na Japan utaendelea kubakia kuwa msingi imara wa diplomasia ya Japan na muhimu kwa uthabiti wa kanda hiyo na dunia kwa ujumla.
Trump, mfanyabiashara bilionea kutoka New York anayetaka ateuliwe na chama chake cha Republican kugombea urais wa Marekani katika uchaguzi wa Novemba 8 pia alisema huenda akasitisha ununuzi wa mafuta kutoka kwa Saudi Arabia na mataifa mengine ya kiarabu yaliyo washirika wake hadi pale yatakapotoa wanajeshi wa ardhini kupambana na kundi la dola la kiislamu au yailipe Marekani kwa kufanya hivyo.
Mwandishi:Josephat Charo/rtre/afp
Mhariri:Iddi Ssessanga