Trump aikosoa NATO katika mazungumzo na Rutte
9 Aprili 2026
Rais wa Marekani Donald Trump ametoa kauli hiyo wakati wa mkutano wa faragha na katibu mkuu wa NATO, Mark Rutte, jana Jumatano katika Ikulu ya White House. Trump alisema amevunjwa moyo na kukatishwa tamaa kwa kuwa NATO haikuwepo wakati Marekani na Israel zilipoanzisha mashambulizi dhidi ya Iran. Uhusiano katika muungano wa kijeshi wa NATO umefikia kwenye hatua ya mgogoro kuhusu vita hivyo vya Iran.
Mataifa kadhaa ya NATO yalisita kuisaidia Marekani katika vita hivyo, kwa kukataa ndege za kivita za Washington kutumia anga zao kuishambulia Jamhuri hiyo ya kiislamu au hata kutuma jeshi la majini kusaidia kuufungua mlango Bahari wa Hormuz, uliofungwa na Iran baada ya vita hivyo kuanza mnamo Februari 28.
Trump mara zote amekuwa akiita Jumuiya hiyo ya NATO kuwa taasisi isiyokuwa na nguvu, na katika wiki za hivi karibuni amekuwa akitishia kuiondoa Marekani katika Jumuiya hiyo iiliyo na wanachama 32, akisema NATO imekuwa ikiitegemea Marekani kwa usalama wake, lakini imeshindwa kuisadia nchi yake pale ilipohitajika.
Licha ya Trump kusema mashambulizi dhidi ya Iran yamesitishwa kwa wiki mbili, mgogoro huo umeendelea kutia doa mahusiano ya nchi yake na washirika wake.
Hapo jana Msemaji wa ikulu ya White HouseKaroline Levitt, alisema mataifa ya NATO yanayopokea usaidizi wa kiulinzi kutoka Marekanani yaliigeuka nchi hiyo pamoja na watu wake.
"Walijaribiwa lakini walishindwa. Na labda ningeongeza, kuwa inasikitisha sana kwamba NATO iliwapa watu wa Marekani kisogo katika kipindi cha wiki sita zilizopita wakati Wamarekani ndio wamekuwa wakifadhili ulinzi wao."
Rutte amekiri badhi ya mataifa ya NATO yalishindwa kutimiza wajibu wao
Kwa upande wake katibu mkuu wa NATO, Mark Rutte, alijibu akisema kwamba anatambua kuwa badhi ya mataifa yalishindwa kutimiza wajibu wao lakini idadi kubwa ya mataifa ya Ulaya yamekuwa yakisaidia katika kuweka kambi za kijeshi, uratibu na mipangilio, kwa kutumia ndege za ziada, na kuhakikisha yanatimiza ahadi zao.
Rutte alikutana na Trump kwa ajili ya majadiliano ambayo yalitarajiwa kuzingatia kuufungua tena mlango bahari wa Hormuz na kutuliza hasira ya Trump dhidi ya Jumuiya hiyo ya NATO kuhusu vita vya Iran.
NATO, inayojumuisha nchi za Ulaya, Marekani na Canada, iliundwa mwaka 1949 kwa lengo la kukabiliana na tishio la mashambulizi ya Umoja wa Kisovieti na kwa miongo kadhaa imekuwa nguzo muhimu ya usalama wa nchi za Magharibi.
Huku hayo yakiarifiwa Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni, ameitolea wito Ulaya na Marekani kufanya kazi pamoja kabla ya ushirikiano wao kuharibika kufuatia vitahivyo vya Iran. Meloni ambaye ni rafiki ya Donbald Trump ameliambia bunge kwamba ni wazi Ulaya iko katika wakati mgumu ikija katika mahusiano yake na Marekani kwahiyo ni lazima wasimame pamoja na kushirikiana kwa karibu zaidi ili kuyatunza mahusiano hayo.