1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Trump akosoa vikali rekodi ya uchumi ya serikali ya Biden

15 Agosti 2024

Mgombea wa urais kupitia chama cha Republican Donald Trump ameikosoa vikali rekodi ya uchumi ya serikali ya Rais Joe Biden akisema imesababisha kupanda kwa gharama za maisha.

Picha ya pamoja | Donald Trump na Kamala Harris
Picha ya pamoja na ya wagombea wa urais nchini Marekani, wakati taifa hilo likakaribia kufanya uchaguzi wake mkuu mwezi Novemba

Donald Trump amesema hayo siku chache kabla mpinzani wake Kamala Harris kuzindua mpango wa kukabiliana na gharama za maisha katika hotuba yake muhimu ya kisera kama mgombea wa urais.

Trump amedai kwamba mpinzani wake huyo wa chama cha Democratic ataibua Mdororo mwingine wa uchumi ikiwa atachaguliwa, huku yeye akiahidi kuongeza ujira na kuboresha tena maisha ya Wamarekani.

Amewaambia wafuasi wake katika eneo la Asheville, katika jimbo la North Carolina kwamba sera kali za Kamala zimesababisha mfumuko wa kutisha wa bei na matatizo mengine ya kifedha kwa watu nchini humo.

Kamala anatarajiwa kuzindua mpango wake huo unaosubiriwa kwa hamu katika mji mkuu wa North Carolina, Raleigh, unaolenga kupunguza gharama za matibabu, nyumba na chakula kwa watu wa kipato cha kati.