Trump aiondolea Uturuki vikwazo
24 Oktoba 2019Akizungumza katika Ikulu ya White House, Trump alisema anaondoa vikwazo hivyo kwa sababu mpango wa kusitisha mapigano ulikuwa ukitekelezwa katika eneo hilo, ambalo Uturuki ilivamia ili kuyafurusha makundi ya wapiganaji wa Kikurdi kutoka kwenye ngome zao.
Trump aliuita mpango huo wa kusitisha mapigano, ambao ulitoa nafasi kwa udhibiti wa Uturuki kuendelea bila kukumbwa na upinzani kwa sehemu kubwa kuwa ni mafanikio makubwa. Aidha ameutetea uamuzi wake wa kuviondoa vikosi vya Marekani nchini Syria, akisema kuwa Marekani haipaswi kuwa polisi ya ulimwengu
"Mataifa ya kanda hiyo lazima yachukue wajibu wa kusaidia Uturuki na Syria kuulinda mpaka wao. Tunataka mataifa mengine yahusike. Mafuta yako salama na hivyo idadi ndogo ya wanajeshi wa Marekani watabaki katika eneo hilo lenye mafuta. Na tutayalinda na tutaamua nini tutayafanyia katika siku za usoni." Alisema Trump
Huku akipinga tuhuma kuwa aliwasaliti Wakurdi wa Syria – ambao waliuawa kwa maelfu wakati wakipigana pamoja na wanajeshi wa Marekani dhidi ya Kundi linalojiita Dola la Kiislamu – IS – Trump alisema wana furaha sana. Amesema kamanda wa Kikurdi nchini humo, Mazloum Abdi alimuambia kuwa wanashukuru sana.
Ujerumani imeyakosoa makubaliano kati ya Urusi na Uturuki ya kuwaondoa wapiganaji wa Kikurdi kutoka eneo la karibu na mpaka wa Uturuki na Syria, kabla ya kuanza mkutano wa ngazi ya juu wa wanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO.
Badala yake, Ujerumani imesisitiza kuhusu umuhimu wa kuwepo na hatua ya kimataifa – kama aliyopendekeza Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Annegret Kramp-Karrenbauer. Msemaji wa Kansela Angela Merkel Steffen Seibert amewaambia wanahabari kuwa Ulaya lazima iyakabili matukio ya sasa yanayoendelea kwenye mpaka wa bara hilo kwa sababu ni maswala ambayo yanaathiri moja kwa moja baadhi ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya.
Kramp-Karrenbauer anatarajiwa kulipigia debe pendekezo lake la kuundwa ukanda wa kimataifa wa usalama kaskazini mwa Syria, katika mkutano wa siku mbili wa mawaziri wa ulinzi wa NATO unaoanza leo mjini Brussels.
Urusi inatarajiwa kushirikiana na Syria kuhakikisha kuwa wanajeshi wa Kikurdi wa YPG wanaondoka katika maeneo ya kaskazini mwa Syria chini ya umbali wa kilomita 30 kutoka mpaka wa Uturuki.