1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump aipa siku nne Hamas kukubali mpango wake wa amani

30 Septemba 2025

Rais Donald Trump wa Marekani amewapa wanamgambo wa Kipalestina siku nne tu wawe wameshakubaliana na mpango wake wa kusitisha mapigano kwenye Ukanda wa Gaza, vyenginevyo akiwatishia kwa kile alichokiita "mwisho mbaya".

USA Washington D.C. 2025 | Donald Trump na Benjamin Netanyahu
Rais Donald Trump wa Marekani (kushoto) amewapa wanamgambo wa Kipalestina hadi Ijumaa wawe wameshakubaliana na mpango wake wa usitishaji mapigano Ukanda wa Gaza.Picha: Jim Watson/AFP

Katika kile kinachoonekana kuwa kitisho cha wazi, Trump aliwaambia waandishi wa habari siku ya Jumanne (Septemba 30), ikiwa ni siku moja tu tangu atangaze mpango huo wenye vipengele 20, kuwa Hamas ilikuwa na siku nne tu za kuukubali mpango huo, vyenginevyo ingekuwa na hali mbaya zaidi.

Aliyasema hayo alipoulizwa na waandishi wa habari alikuwa anatazamia lini mpango huo ungeanza kutekelezwa. 

"Tutalifanikisha hili kwa siku tatu ama nne kutoka sasa. Nchi zote za Kiarabu zimekubali. Nchi za Kiislamu zote zimekubali. Israel imekubali . Tunawangojea Hamas tu, ama watakubali au watakataa. Na kama wakikataa, watakuwa na mwisho mbaya sana." Alisema rais huyo wa Marekani, ambaye amekuwa muungaji mkono mkubwa wa Israel.

Urusi, ambayo kawaida huwa haijihusishi sana na mzozo huo wa Mashariki ya Kati, imesema ingawa haikushirikishwa kwenye mpango huo wa Trump, lakini inauunga mkono na inatarajia utapelekea sululisho la amani kwa pande zote zinazohusika.

Hamas waujadili mpango wa Trump

Kwa upande wake, kundi la Hamas lilisema limeyapokea na sasa linayajadili mapendekezo yaliyomo kwenye mpango wa Trump  wa kusitisha mapigano kwenye Ukanda wa Gaza. 

Mpango huo uliotangazwa jana, tayari unaungwa mkono na Israel na mataifa kadhaa ya Kiarabu na Ulaya yanayosema unatowa mwanga wa kukomesha miaka miwili ya umwagaji damu kwenye Ukanda huo. 

Mahojiano: Mpango wa Trump kwa Gaza

This browser does not support the audio element.

Qatar, ambayo ni mmojawapo wa wapatanishi wakuu watatu wa mzozo huo, imesema wajumbe wake wanakutana Jumanne ya leo na wale wa Hamas na Uturuki, nchi ambayo imeombwa na Hamas kuwa sehemu ya wapatanishi, kuujadili mpango huo wa Trump.

Wapalestina 27 wauawa Gaza

Mamlaka za afya kwenye Ukanda wa Gaza zilisema ndani ya kupindi cha masaa 24 yaliyopita, watu 27 walikuwa wameuawa kwenye kitovu cha Jiji la Gaza, ambako Israel imekuwa ikiendeleza operesheni yake inayodai kulenga kuliangamiza kabisa kundi la Hamas na kuwakomboa mateka wake waliosalia huko. 

Kwenye uchochoro wa Netzarim unaodhibitiwa na jeshi la Israel, ambao unayaunganisha maeneo ya kaskazini na kusini mwa Gaza, Wapalestina 17 wameuawa na wengine 33 kujeruhiwa walipokuwa wakijaribu kufikia eneo linalogaiwa msaada wa chakula.

Mashambulizi ya Israel yakiendelea kwenye Ukanda wa Gaza licha ya tangazo la mpango wa amani wa Trump.Picha: Jack Guez/AFP/Getty Images

Kwenye tukio jengine, mashambulizi mawili ya anga dhidi ya mahema ya wakimbizi wa ndani katika eneo la Muwasi, jeshi la Israel limewauwa Wapalestina wengine 10, saba kati yao wameuliwa kwenye kitongoji cha Deir al-Balah ambao ni sehemu ya wale waliokimbia eneo la kaskazini mwezi huu baada ya kuamriwa kufanya hivyo na jeshi.

Watatu wengine wa familia moja: mume, mke mwenye uja uzito wa miezi saba na mtoto wao, wameuawa kwenye kitongoji cha Khan Younis wakiwa kwenye hema lao.

Wizara ya Afya ya Gaza imesema kufikia sasa watu waliokwishauawa tangu mashambulizi ya Israel mwezi Oktoba mwaka 2023 imefikia 66,000 huku wengine 170, 000 wakijeruhiwa. Israel ilianzisha mashambulizi hayo kulipiza kisasi uvamizi wa wanamgambo wa Kipalestina kusini mwa nchi hiyo uliopelekea vifo vya zaidi ya watu 1,200 na wengine zaidi ya 200 kuchukuliwa mateka.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW