1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Trump ajitetea, adai Wademocrat waihujumu azma yake ya urais

5 Aprili 2023

Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump amejitetea vikali katika matamshi yake ya kwanza kwa umma tangu kufikishwa kizimbani Jumanne.

USA | New York | Ex-Präsident Donald Trump
Picha: Evan Vucci/AP Photo/picture alliance

Rais huyo wa zamani amefikishwa mahakamani kwa mashtaka ya kumlipa mwanamke mmoja nyota wa filamu za ngono kabla uchaguzi, ili asizungumzie uhusiano wa kingono waliokua nao. Trump amewakosoa waendesha mashtaka nchini humo akisema  "wameitusi nchi hiyo."

Muda mfupi baada ya kuwasili huko Mar-a-Lago, Florida, baada ya kurudi kutoka New York alikokanusha mashtaka ya jinai dhidi yake, Trump aliuhutubia umati wa wafadhili, marafiki zake wa kisiasa na wafuasi wake akisema hakudhani kwamba kitu kama yeye kufunguliwa mashtaka, ni jambo ambalo lingewahi kutokea nchini Marekani.

Wafuasi wa Trump wakimshangilia huko FloridaPicha: Paul Hennessy/AA/picture alliance

Mstari wa mbele kuiwania tiketi ya chama cha Republican

Trump amejitetea akisema hajafanya kosa lolote na kwamba mashtaka dhidi yake yanastahili kuondolewa mara moja. Anadai kuwa kosa lake kubwa lilikuwa kuitetea Marekani kutoka kwa wale wanaonuia kuiharibu.

"Kuanzia mwanzo Wademocrat walikuwa wanachunguza kampeni yangu, mnakumbuka? Walinishambulia kwa kufanya uchunguzi wa uongo, Urusi, Urusi, Urusi, Ukraine Ukraine, Ukraine, uongo wa kwanza wa kuniondo madarakani, uongo wa pili wa kuniondoa madarakani, uvamizi wa makaazi yake ya Mar-a-lago hapa," alisema Trump.

Rais huyo wa zamani ambaye anapigiwa upatu kuipeperusha bendera ya chama cha Republican katika kuwania urais kwenye uchaguzi wa mwaka 2024 amesema waendesha mashtaka kote nchini humo wanatumia kila mbinu ili wampate na hatia.

Amemshambulia mwendesha mashtaka wa Manhattan Alvin Bragg anayeiongoza kesi hiyo akisema hajui lolote kumhusu na jaji anayeisikiliza hiyo kesi Juan Merchan naye, hakusazwa na Trump kwani amesema jaji huyo ni "jaji anayemchukia Trump."

Masaa machache kabla, rais huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 76 alikanusha mashtaka 34 dhidi yake katika mahakama ya New York, katika tukio ambalo lilikuwa la kihistoria kwani Trump ndiye amekuwa rais wa kwanza wa zamani Marekani kufunguliwa mashtaka ya jinai.

Waendesha mashtaka wanasema Trump alidanganya mara kadhaa kuhusu rekodi zake za biashara mjini New York ili kuficha taarifa ambazo zingemchafulia jina kwa wapiga kura katika uchaguzi wa mwaka 2016 alioushinda.

"Chini ya sheria za jimbo la New York, ni kosa kubwa kudanganya kuhusu rekodi za biashara kwa lengo la kutapeli na kuficha uhalifu mwengine. Kesi hii inahusu mambo haya. Taarifa 34 za uongo zilizotolewa ili kuficha uhalifu mwengine. Huu ni uhalifu mkubwa katika jimbo la New York. Hatujali wewe ni nani, unapofanya uhalifu hatuwezi kuuchukulia kama jambo la kawaida," alisema Bragg.

Afisa wa zamani wa Trump anahudumia kifungo jela kwa makosa sawa na hayo

Afisa mkuu wa zamani wa masuala ya fedha wa Trump Allen Weisselberg, kwa sasa anahudumia kifungo cha miezi mitano jela kwa makosa kama hayo ya kutoa rekodi za uongo za biashara.

Trump akiwa mahakamani New YorkPicha: Timothy A. Clary/Pool Photo/AP/picture alliance

Trump anatuhumiwa kuwalipa wanawake wawili kabla uchaguzi wa mwaka 2016 ili kuwanyamazisha wasitoe taarifa kuhusiana na mahusiano yao ya kingono. Wanawake hao wawili walikuwa Stormy Daniels, nyota wa filamu za ngono na mwanamtindo wa zamani Karen McDougal.

Jaji Juan Merchan amesema kesi hiyo itasikilizwa mnamo Desemba 4, ingawa wanasheria wanadai huenda hata mwaka ukaisha kabla haijasikilizwa. Wanasheria hao wanasema vile vile kufunguliwa mashtaka au hata kuhukumiwa, kisheria hakutomzuia Trump kugombea kiti cha urais.

Chanzo: Reuters/AFP

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW