Trump ajitosa katika jitihada za kutafuta amani Sudan
20 Novemba 2025
Donald Trump, alisema jana Jumatano kuwa atatoa uzito zaidi katika kusaidia kuumaliza mzozo mbaya wa Sudan. Amesema alizungumza kwa kina zaidi kuhusu vita hivyo katika mazungumzo aliyoyafanya na Mwanamfalme wa Saudi Arabia, Mohammed Bin Salman katika ikulu ya Marekani, White House.
Akizungumza katika mkutano wa pamoja na mgeni wake huyo kabla ya Bin Salman kuhitimisha ziara yake Marekani, Trump amesema, "Nimeshasuluhisha mizozo minane na Mwanamfalme angependa nifanye kitu kikubwa kuhusu Sudan. Haikuwa kwenye mawazo yangu kuhusika kwenye vita hivi lakini ninaona ilivyomuhimu kwako na marafiki zako kwenye chumba hiki. Tutaanza kuifanyia kazi Sudan."
Baada ya kauli hiyo, Trump kupitia chapisho aliloliweka kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii, ameongeza kuwa utawala wake utashirikiana na Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Misri na washirika wengine wa Mashariki ya Kati ili kuyamaliza madhila yanayoendelea wakati wakiimarisha Sudan.
Matamshi hayo ya Trump yametolewa baada ya Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Marco Rubio kutoa wito wa kusitisha msaada wa kijeshi unaotoka nje ya Sudan kwenda kwa wanamgambo wa RSF.
Vifo vyazidi kuripotiwa El Fasher, maelfu wakimbia
Hivi karibuni, wanamgambo hao waliudhibiti mji mkuu wa Dafur Kaskazini waEl Fasher na kusababisha mamia ya vifo. Kulingana na maafisa wa Umoja wa Mataifa na mashirika ya wahisani, zaidi ya wakaazi 90,000 wa mji huo na maeneo jirani wamelazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na ukatili unaoripotiwa kufanywa na RSF.
Vita vya Sudan vilivyoibuka April 2023 hadi sasa vimeshasababisha vifo vya zaidi ya watu 40,000. Maafisa wa Saudi Arabia wanasema kuwa kwa kiasi fulani, kuendelea kwa mzozo wa Sudan kunaweza kusababisha kukosekana kwa utulivu katika Bahari ya Shamu na Afrika.
Hali hiyo inahofiwa kutengeneza mazingira yatakayowasaidia wanamgambo wenye itikadi kali kueneza ugaidi Mashariki ya Kati na kwingineko.
Vita hivyo kati ya jeshi rasmi lililo chini ya Jenerali Abdel Fattah Burhan na kundi la RSF linaloongozwa na Mohamed Hamdan Dagalo vimeyagawanya baadhi ya mataifa makubwa.
Misri, Uturuki na Saudi Arabia zinatajwa kuliunga mkono jeshi wakati Umoja wa Falme za Kiarabu na mshirika wake Marekani wakidaiwa kuwapatia silaha wanamgambo wa RSF kwa mujibu wa taarifa za kiintelijensia za Marekani.