1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump akamilisha ziara yake barani Asia

Isaac Gamba
13 Novemba 2017

Rais wa Marekani Donald Trump anakamilisha ziara yake ndefu barani Asia kwa kushiriki mkutano wa kilele wa Jumuiya ya ushirikiano ya maendeleo ya nchi za mataifa ya kusini mashariki mwa Asia (ASEAN).

Philippinen ASEAN Gipfel in Manila
Picha: Getty Images/AFP/J. Watson

Trump hii leo  amekutana na waziri mkuu wa Austrialia Malcom Turnbull ambaye alifanya naye mazungumzo kwa njia ya simu wakati wa majira ya baridi yaliyopita pamoja na waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe  aliyekuwa mwenyeji wake mjini Tokyo mwanzoni mwa ziara yake barani Asia.

Rais  huyo wa Marekani ambaye hii ni ziara yake ya kwanza barani Asia tangu aingie madarakani alizungumzia juu ya ziara yake katika mataifa matano barani Asia iliyohusisha masuala ya kibiashara pamoja na suala la Korea Kaskazini lakini akaongeza kuwa atafafanua zaidi mara baada ya kurejea Marekani ambapo atatoa tamko zito kuhusiana na ziara yake hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Manila Trump alisema wamepiga hatua kubwa zaidi kuhusiana na masuala ya kibiashara ikiwa ni pamoja na mikataba mikubwa ya kibiashara kati ya Marekani na makampuni ya kigeni.

 

Trump asifia mapokezi yake barani Asia

Rais wa Marekani Donald Trump pamoja na rais wa Ufilipino Rodrigo DutertePicha: Reuters/J. Ernst

Aidha alisifia mapokezi makubwa aliyoyapata  mjini Tokyo, Seul na Beijing wakati wa ziara yake hiyo barani Asia akisema yalikuwa ni mapokezi yenye hadhi ya juu na yenye heshima kubwa  na kuwa anajivunia mapokezi hayo kwa heshima yake na kwa Marekani kwa ujumla.

Hafla ya ufunguzi ya mkutano wa Jumuiya ya ushirikiano ya maendeleo ya nchi za mataifa ya kusini mashariki barani Asia (ASEAN) ilianza kwa shamra shamra ikiwa ni pamoja na picha ya pamoja ya viongozi wanaoshiriki mkutano huo  ambapo walishikana mikono kama ilivyo ada wakati wanapokutana katika mikutano ya aina hiyo.

Katika hafla fupi na waandishi wa habari Trump alisema kuwa yeye na rais Duterte wamekuwa na na mahusiano mazuri ingawa alikwepa kujibu maswali iwapo aliibua swala linahusiana na haki za binadamu katika mazungumzo yake na rais  Duterte.

Kwa mujibu wa ikulu ya Marekani White House katika kiao chao kilichodumu kwa dakika 40 viongozi hao wawili walijadili juu ya masuala yanayolihusu kundi la itikadi kali la Dola la Kiisilamu, madawa ya kulevya pamoja na masuala yanayohusu biashara huku msemaji wa ikulu ya Marekani Sarah Huckabe Sanders akisema suala linalohusiana na haki za binadamu lililitajwa wakati wa mazungumzo yaliyohusu operesheni ya Ufilipino dhidi ya madawa ya kulevya.

 Rais Trump ambaye pia anatarajia kukutana na waziri mkuu wa India Narendra Modi aligusia pia suala linalohusiana na Urusi kuingilia uchaguzi wa Marekani mwaka jana na kusema kuwa  ingawa rais wa Urusi Vladimir Putin amekuwa akisisitiza kuwa yeye binafsi na urusi hawakuingilia uchaguzi huo  lakini yeye  Trump anayaamini mashirika ya ujasusi ya Marekani wakati yanaposema kuwa Urusi iloingilia uchaguzi huo wa mwaka jana.

Mwandishi: Isaac Gamba/ape

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman