1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMarekani

Trump akanusha taarifa za onyo kuhusu kuishambulia Iran

24 Februari 2026

Rais wa Marekani Donald Trump amekanusha vikali taarifa za vyombo kadhaa vya habari vya Marekani vilivyodai kwamba Jenerali Dan Caine aliwaonya viongozi wa juu wa Marekani kuhusu hatari za kuishambulia Iran.

USA Washington D.C. 2026 | Donald Trump
Rais wa Marekani Donald Trump akizungumza na waandishi wa habari katika Ikulu ya White HousePicha: Kevin Lamarque/REUTERS

Kwa mujibu wa ripoti hizo, Caine alionyesha wasiwasi kuhusu uwezekano wa mgogoro wa muda mrefu, uhaba wa silaha, kupungua kwa ulinzi wa anga na vifo kwa wanajeshi wa Marekani na washirika wake iwapo Washington itaishambulia Tehran. 

Vyombo kadhaa vya habari vya Marekani vimeripoti kwamba Jenerali Dan Caine, Mwenyekiti wa Wakuu wa Majeshi ya Pamoja, alitoa onyo kuhusu hatari za mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran.

Gazeti la The Washington Post liliripoti kwamba Caine alikuwa ameonyesha wasiwasi juu ya uhaba wa silaha na uwezekano wa kukosa uungwaji mkono wa washirika, jambo ambalo lingeongeza hatari kwa wanajeshi wa Marekani.

Nalo Gazeti la Wall Street Journal liliandika kwamba, maafisa kadhaa wa Pentagon, akiwemo jenerali huyo wa jeshi,  walionya kuhusu athari ambazo zinaweza kujitokeza ikiwemo vifo kwa wanajeshi wa Marekani na washirika wake, pamoja na kupungua kwa uwezo wa ulinzi wa anga wa Marekani iwapo mashambulizi yangefanyika.

Chombo cha habari cha Axios, kwa upande wake, kimeripoti kwamba Caine alikuwa ameonya kuhusu Marekani "kunaswa katika mgogoro wa muda mrefu."

Kwa mujibu wa Axios, baadhi ya watu wa karibu na Rais Trump akiwemo mjumbe wake maalum katika masuala ya Mashariki ya Kati Steve Witkoff na mkwe wake Jared Kushner wamemshauri atumie diplomasia badala ya kufanya mashambulizi ya kijeshi.

Marekani imepeleka majeshi katika eneo la Mashariki ya Kati kufuatia kile maafisa wake wamekitaja kuwa "ongezeko la vitisho" kutoka kwa IranPicha: Daniel Kimmelman/US Navy/AFP

Licha ya vyombo hivyo vya habari kuripoti kuhusu onyo alilolitoa afisa huyo mkuu wa jeshi la Marekani, Trump amekanusha vikali taarifa hizo na kuvishtumu vyombo hivyo vya habari kwa kuandika habari zisizokuwa sahihi kwa makusudi.

Kupitia ujumbe aliouandika katika mtandao wa Truth Social, kiongozi huyo wa Marekani amesema, "Mimi ndiye ninayefanya maamuzi, ningependelea kupata makubaliano kuliko kutoyapata lakini, tusipopata makubaliano, itakuwa siku mbaya sana kwa Iran na kwa masikitiko makubwa, kwa watu wake."

Trump ameongeza kwamba jenerali Caine hajawahi kumpinga kuhusu suala la Iran na kwamba Marekani ina uwezo wa kuishinda Iran "kwa urahisi” endapo vita vitatokea.

Trump ambaye aliwahi kuagiza mashambulizi dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran mwaka uliopita, na tangu wakati huo amekuwa akitoa vitisho vya kijeshi endapo mazungumzo ya sasa hayatafanikiwa.

Marekani na Iran zinafanya mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran ambao kwa mingi umekuwa chanzo cha mvutano kati ya Tehran na Washington.

Kwa mujibu wa vyanzo rasmi vya serikali ya Marekani, duru nyingine ya mazungumzo inatarajiwa kufanyika Geneva siku ya Alhamisi.

Wakati hayo yakiripotiwa, Trump anatarajiwa hii leo kutoa hotuba yake mbele ya bunge kuhusu hali ya taifa katika wakati ambapo uungwaji mkono kwake uko katika kiwango cha chini kuliko kawaida.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW