Trump akanusha Urusi kuingilia uchaguzi wa Marekani
4 Agosti 2017Trump ameyasema hayo katika mkutano uliofanyika Huntington Virginia na kusisitiza kuwa madai hayo ni ya uzushi na ni kisingizio kutokana na wapinzani wake kutokuwa na hoja ya kusema au malengo baada ya kushindwa uchaguzi.
Trump ameongeza kuwa Watu wengi wanajua fika kuwa hakukuwa na warusi katika kampeni zao na kuwa hawakushinda kwasababu ya Urusi ila walishinda kwa sababu ya wapiga kura kuwachagua.
Vyombo vya habari vimeripoti kuwa kiongozi wa tume maalumu ya uchunguzi Robert Mueller ameunda jopo la majaji kuchunguza sakata hilo njia ambayo waendesha mashitaka hupata nyaraka au hulazimisha mashahidi kutoa ushahidi kuhusaiana na kesi muhimu za kijinai.
Baadhi ya majaji wanaofuatilia tuhuma hizo katika wiki za hivi karibuni walikuwa wakitafuta nyaraka zinazohusiana na masuala ya kibiashara yanayomhusu Michael Flynn , aliyekuwa mshauri wa kitaifa katika masuala ya usalama wa Rais Trump. Hiyo ni kwa mujibu wa gazeti la New York Times katika taarifa yake likiwanukuu wanasheria wanaofuatilia tuhuma hizo.
Jarida la Wall Street mapema liliripoti kuwa kiongozi maalumu anayechunguza madai ya Urusi kuingilia uchaguzi mkuu wa Marekani wa mwaka jana alikuwa tayari ameunda jopo hilo la majaji kufuatilia tuhuma hizo. Jopo la majaji hujumuisha raia wa kawaida ambao wanaweza kuamua kutoa hati ya kuitwa kuhojiwa na mashauri ya aina hiyo huendeshwa kwa faragha.
Michael Flyn aliyejiuzulu mwezi Februari mwaka huu baada ya kukiri kutoa taarifa zisizojitosheleza kuhusiana na mawasialiano kati yake na balozi wa Urusi nchini Marekani Sergei Kislyak naye pia ameitwa na jopo la majaji la Virginia pamoja, kamati ya baraza la seneti na ile ya baraza la wawakilishi.
Shirika la habari la CNN limeripoti kuwa jopo lingine la majaji lililoundwa kufuatilia sakata hilo liliitisha nyaraka kutoka kwa watu waliohusika katika vikao vilivyomkutanisha mtoto wa kiume wa Rais Trump, Trump Juniour na mwanasheria wa Urusi.
Mwanasheria wa Trump amesema hakuwa na taarifa kuhusiana na jopo la majaji lililoundwa kufuatilia kadhia hiyo kama ilivyoripotiwa na jarida la Wall Street lakini akasema ikulu ya White House itaendelea kushirikiana na Mueller kiongozi mkuu wa uchunguzi huo.
Kamati ya baraza la seneti pamoja na ile ya baraza la wawakilishi pamoja na tume huru wanachunguza iwapo kulikuwa na makubaliano kati ya wajumbe wa timu ya kampeni ya Trump na Urusi katika kujaribu kushawishi matokeo ya uchaguzi mkuu wa Novemba mwaka jana.
Mashirika ya ujasusi ya Marekani yanasisitiza kuwa Urusi ilifanya udukuzi wa barua pepe za chama cha Democratic kwa madhumuni ya kumfanya Hillary Clinton mgombea wa chama cha Democratic asishinde uchaguzi huo.
Waendesha mashitaka wameonyesha wasiwasi wao kuwa Rais Trump anaweza akaingilia uchunguzi huo unaoongozwa na Mueller au atafute njia za kumfuta kazi.
Hata hivyo maseneta wawili hii leo wamewasilisha muswada ambao utafanya iwe vigumu kwa Rais kufanya hivyo.
Mwandishi: Isaac Gamba/DPAE
Mhariri: Iddi Ssessanga