Trump akasirishwa na FBI kuzipekua ofisi za Cohen
10 Aprili 2018Maafisa wa Shirika la Upelelezi la Marekani, FBI wamezipekua ofisi za wakili binafsi wa Rais wa Marekani Donald Trump, Michael Cohen. Trump amekasirishwa na hatua hiyo na kulikosoa vikali shirika hilo.
Stephen Ryan, ambaye ni wakili wa Cohen, amesema kuwa upekuzi huo uliofanyika jana ni sehemu ya maelekezo kutoka kwa Robert Mueller, mwanasheria anayeoongoza uchunguzi kuhusu ushirikiano kati ya timu ya kampeni ya Rais Trump pamoja na Urusi wakati wa uchaguzi wa urais uliofanyika Marekani mwaka 2016.
Hata hivyo, gazeti la The New York Times limeripoti kuwa uvamizi huo hauhusiani na maelezo ya Mueller. Ryan ametoa taarifa inayoeleza kuwa mteja wake tayari alishirikiana na maafisa kwa kuwasilisha maelfu ya nyaraka kwa wachunguzi wa bunge, ambao pia wanachunguza kuhusu madai ya Urusi kuingilia uchaguzi wa Marekani.
Aidha, Ryan amekosa uvamizi huo wa FBI akisema kuwa matumizi ya vibali vya kufanya uchunguzi hayakuwa sawa na hayakufaa kabisa. Amesema katika upekuzi huo maafisa wa FBI wamechukua taarifa kuhusu matukio mbalimbali ikiwemo nyaraka za malipo ya Dola 130,000 yaliyotolewa kwa mcheza filamu za ngono, Stormy Daniels.
Cohen na Mueller wote hawajazungumza lolote kuhusu sakata hilo. Akizungumza na waandishi habari, Trump amelaani vikali uvamizi huo na kusema kwamba uchunguzi unaofanywa na Mueller ni shambulizi dhidi ya Marekani.
''Nimesikia kwamba wamevamia ofisi ya mmoja wa mawakili wangu binafsi, mtu mzuri. Hali hii ni ya aibu. Ni shambulizi dhidi ya nchi yetu, kwa maana halisi. Ni shambulizi katika kile ambacho sisi wote tunakisimamia,'' alisema Trump.
Katika wiki za hivi karibuni, Cohen ametawala katika vyombo vya habari tangu ilipogundulika kuwa alimlipa Dola 130,000 Stormy Daniels kabla ya uchaguzi wa urais mwaka 2016. Daniels alisema fedha hizo zilikuwa ni malipo ya kumnyamazisha na asizungumze chochote kuhusu madai kwamba alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Trump.
Hata hivyo, Ikulu ya Marekani imeyakanusha madai ya Daniels na Rais Trump amesema hajui lolote kuhusu malipo hayo yaliyotolewa na Cohen. Uvamizi huo ni mtihani mwingine kwa Trump wakati ambapo yeye na mawakili wake wanaangalia iwapo wakubaliane kuhusu kuhojiwa na timu ya Mueller, ambayo inachunguza madai ya uhusiano kati ya Urusi na Marekani.
Kulingana na masharti na kanuni za wizara ya sheria ya Marekani, Mueller anapaswa kushauriana na Naibu Mwanasheria Mkuu Rod Rosenstein, iwapo wachunguzi wake watabaini ushahidi mpya ambao unaweza kuangukia nje ya mamlaka yake ya awali. Baada ya hapo Rosenstein ataamua kama amruhusu Mueller kuendelea au kumpa jukumu hilo mwanasheria mwingine wa Marekani au mtu mwingine ambaye ni sehemu ya wizara ya sheria.
Kwa mujibu wa The New York Times, timu hiyo maalum ya Mueller inachunguza pia malipo ya Dola 150,000 yaliyotolewa wakati wa kampeni za uchaguzi wa urais wa Marekani kwa bilionea wa Ukraine, Viktor Pinchuk. Fedha hizo zililipwa na mfuko wa Trump wa mradi wa mali zisizohamishika ili uweze kupewa muda wa dakaki 20 kuhutubia kwa njia ya video kupitia mfumo maalum wa kuwaunganisha watu kutoka maeneo mbalimbali.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AP, AFP, DW https://bit.ly/2qi6VZq
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman